KUELEKEA FAINALI YA UEFA ... MAMBO 14 MUHIMU KUYAFAHAMU KATI YA SIMEONE NA ZIDANE

Unknown | 2:14 PM | 0 comments


Kesho Mei 28 katika dimba la San Siro, kutakuwa na pambano kali la fainali ya UEFA pale Real Madrid watakapokuwa wakichuana na mahasimu wao wakubwa Atletico Madrid. Hii imekuwa ni fursa adhimu sana kwa makocha wa timu zote mbili yaani Zinedine Zidane na Diego Simeone kuoneshana umwamba kutokana na wote kuwa na historia ya kuvichezea vilabu hivyo.

Kwa kufahamu umuhimu wa pambano hili, tumeamua kukuletea baadhi ya mambo muhimu ya kukumbukwa kati ya makocha hawa hawa kuelekea pambano hili;

Diego Pablo Simeone (El Cholo) amewahi kuitumikia Atletico Madrid kama mchezaji katika vipindi viwili tofauti (1994-97 na 2003-05).

Zinedine Zidane alijiunga na Real Madrid kama mchezaji katika dirisha kubwa la usajili la majira ya joto mwaka 2001 na kudumu kwa miaka mitano mpaka msimu wa mwaka 2005-06 alipoamua kustaafu soka.

Zidane aliichezea Real almaarufu Blancos michezo 227, akifunga mabao 49 na kubeba makombe sita ,likiwemo la UEFA ambapo alifunga goli la kipekee baada ya kupiga mpira aina ya ‘volley’ katika fainali dhidi ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani mwaka 2002.

Simeone alikuwemo ndani ya kikosi cha kukumbukwa cha Atletico kilichochukua kwa pamoja La Liga na Copa del Rey mwaka1996. Tangu achukue mikoba ya kuwa kocha amefanikiwa kubeba makombe matano na kuongeza idadi ya makombe katika klabu hiyo – La Liga, Copa del Rey, Supercopa mawili na ligi ya Europa.

Derby ya kwanza ya Zidane ilikuwa ni Januari mwaka 2003 pale timu hizo zilipotoshana nguvu kwa kufungana magoli 2-2.

Kipigo kikubwa cha Simeone akiwa kama mchezaji wa Atletico kilikuwa ni Desemba mwaka 1994 ambapo Atletico walifungwa mabao 4-2.

Desemba 3, 2003, Zidane na Simeone walikutana kama wachezaji wa Real na Atletico katika dimba la Santiago Bernabeu. Magoli ya Ronaldo de Lima na Raul Gonzalez yalihitimisha ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Atletico Madrid.

Machi 4, 2006, Zizou alicheza mechi yake ya mwisho dhidi ya  Atletico. Katika mchezo huo Real Madrid walishinda mabao 2-1.

Baada ya kushindwa kuwaonesha umwamba Real Madrid wakati akiichezea Atletico, akiwa kama kocha Simeone amebadili kabisa upepo wa Atletico, amekuwa akiifunga Real kadri anavyojisikia.
Mchezo wa kwanza kwa Zidane kama kocha mkuu wa Real Madrid ulikuwa dhidi ya Deportivo la Coruna.

Kipigo cha mabao 4-1 Atletico walichokipata dhidi ya Real, ndiyo ilikuwa ‘derby’ ya kwanza kwa Simeone akiwa kama kocha. Mchezo huo ulipigwa April 2012 katika dimba la Vicente Calderon.

Zidane, alionja ladha ya ubingwa akiwa kama kocha msaidizi wa Carlo Ancelotti mwaka 2014 katika fainali ya UEFA baada ya Real Madrid kuinyuka Atletico mabao 4-1. Mchezo huo ulipigwa Lisbon Ureno.

El Cholo amewahi kuchukua makombe mbele ya Real Madrid wakati wa fainali. Amechukua Copa del Rey na Supercopa.

Derby ya kwanza ya Zidane akiwa kama kocha alipokea kipigo cha bao 1-0 katika dimba la Santiago Bernabeu, moja kati ya mchezo wa ovyo alioshuhudia timu yake ikicheza tangu alipoanza kuifundisha Real.

Na hatimaye sasa, Zidane na Simeone wanakutano kesho katika fainali ya UEFA wote wakitaka kulipiza kisasi kwa namna ya tofauti. El Cholo akitaka kulipiza machungu ya kipigo cha mwaka 2014 cha magoli 4-1 kutoka kwa Real, wakati Zidane kuonesha umwamba akiwa kama kocha Mkuu wa Madrid katika fainali yake ya kwanza na kuwapa ubingwa baada ya kufanya hivyo mwaka 2014 akiwa kama kocha msaidizi.

Yote kwa yote, hii inatarajiwa kuwa ni fainali ya aina yake kutokana na makocha wote wawili kufahamiana vilivyo ndani na nje ya uwanja. Diego Simeone akitegemea hamasa, ari na nguvu kutoka kwa wachezaji kuipa ushindi timu yake, huku Zidane akitegemea zaidi ubora wa mastaa wake kama Ronaldo na Bale ili kuamua matokeo ya mchezo.

Yetu macho, kesho ndiyo kesho ama El Cholo au Zizzou, atakayechanga karata zake vizuri ndiye ataibuka mshindi na kutwaa ndoo ya UEFA kwa mara ya kwanza katika historia zao za maisha yao ya ukocha.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments