NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta hatashiriki kambi ya wiki moja ya timu hiyo nchini Misri, na badala yake atajiunga na wenzake Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Lesotho.

Taifa Stars watamenyana na Lesotho Juni 10, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa.

Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Samatta hataiwahi kambi ya Misri kwa sababu anakabiliwa na majukumu katika klabu yake, KRC Genk nchini Ubelgiji.

Msangi amesema kwamba, kiungo Farid Malik Mussa atajiunga na timu nchini Misri akitokea Hispania anakochezea DC Tenerife ya Daraja la Kwanza, ingawa bado anakomazwa kikosi cha pili. 

Kama Ulivyosikia ndivyo ilivyotokea kwa mara nyingine tena katika Historia ya Ligi kuu Soka Tanzania Bara,Mabingwa Watetezi Yanga wanatwaa kwa mara nyingine ubingwa wa ligi kuu msimu huu kwa kuwafunga Toto Africans ya Mwanza.

Yanga imeibuka na ushindi wa bao 1-0 jioni hii katika dimba la Taifa jijini katika mchezo ambao kuna baadhi ya wadau wa Soka walikua wakidhani pengine Yanga wangewaachia Toto Africans ili kuwanusuru na janga la kushuka daraja linalowakabili.

Amiss Tambwe ameingia katika vitabu vya kumbukumbuku ya ubingwa wa Yanga msimu huu akifunga bao pekee kwa kichwa dakika ya 82 ya mchezo bao ambalo liliwanyima raha kabisa Toto ambao walionekana kuwabana vyema Yanga dakika zote za mchezo.

Kwa Matokeo haya Yanga wanafikisha pointi  68 huku wakiwa na mtaji mkubwa wa magoli ya kufunga na kufungwa tofauti ya magoli 44 wakiwa wamebakiza mechi moja sawa a wapinzani wao Simba na njia pekee ya Yanga kuzuiwa ubingwa huu ni  kufungwa katika mechi ya mwisho kwa idadi kubwa ya magoli pia Simba washinde kwa magoli zaidi ya 12-0 jambo ambalo linaonekana kama ni kitendawili.

Kazi kubwa sasa wanayo Toto Africans na inawezekana kabisa wakashuka daraja baada ya mechi ya Mwisho kwani mpaka sasa wana pointi 29 nafasi ya pili toka mkiani mwa Msimamo wa ligi.
JUMA KASEJA-KAGERA SUGAR.

ZIKIWA zimesalia mechi chache kabla ya kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2016/17, wapo magolikipa waliofanya vizuri mpaka sasa.

Ingawa msimu huu haukuwa na kiwango kikubwa cha makipa wapya kuibuka na kuteka hisia za mashabiki au baadhi ya viongozi wa timu kubwa kuanza kuwamezea mate, wale wa zamani wameonekana kuokoa jahazi.

Makipa wengi wa Ligi Kuu msimu huu wameonekana kuwa ni wa kawaida sana, wakiwa na makosa mengi, wakifungwa mabao rahisi, pia wakishindwa hata kupanga mabeki wao sawasawa, wakati wanashambuliwa au kupigiwa mipira ya faulo.

Wafuatao ni makipa ambao wao angalau wameitoa kimasomaso Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuonekana kufanya vema langoni.

1. Juma Kaseja-Kagera Sugar
Kwa zaidi ya miaka 17 sasa bado anacheza Ligi Kuu Tanzania Bara, tena kwa kiwango cha juu.

Ingawa umri unamtupa mkono na si kama Kaseja yule wa miaka ya 2000, lakini uwezo huu tu alionao, amewashinda makipa wengi vijana ambao kwa sasa walitakiwa wawe kama yeye alivyokuwa huko nyuma.

Pamoja na kusajiliwa kipindi cha dirisha dogo katikati ya msimu, lakini mechi chache tu alizocheza, bado amekuwa na uwezo mkubwa kuzuia michomo ya wachezaji wa timu pinzani, bado ni mwepesi kuruka, lakini pia hafungwi mabao ya kizembe.

Wengi walithibitisha hivyo kwenye mechi kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba.

Lakini tangu alipojiunga, ameifanya timu ya Kagera Sugar kuwa iliyofungwa mabao machache zaidi.

Ndiyo maana haikuwa ajabu alipochaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu wa mwezi Januari.

Kama makipa vijana wataendelea kuonyesha udhaifu wao, Kaseja huyo na ukongwe wake anaweza kugombaniwa na klabu kubwa, pia kucheza zaidi ya misimu mitatu mingine kwa kukosa changamoto kutoka kwa vijana.

2. Deogratius Munishi 'Dida'-Yanga
Ni mmoja kati ya makipa wazoefu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuzichezea klabu za Simba, Mtibwa Sugar, Azam FC na sasa Yanga. Ndiye kipa namba moja wa Yanga. Ni kipa aliyechangia kwa kiasi kikubwa Yanga kucheza mechi za kimataifa na kuwapo hapa ilipo katika Ligi Kuu na Kombe la FA.

Amekuwa akiiokoa timu yake kufungwa hata kwenye mechi ambazo mabeki wa timu hiyo wanakatika au hawako vizuri siku hiyo.

Ni mmoja kati ya makipa waliofanya vizuri sana msimu huu.

3. Aishi Manula-Azam
Bado anaendelea kuwa mmoja wa makipa bora vijana kwenye soka la Tanzania.

Wakati Kaseja na Dida wanaelekea ukingoni, Manula anabaki kuwa hana mshindani wa kweli wa kumpa presha kwenye eneo lake hilo, hasa kwa makipa wazawa.

Ameendelea kuwa na ubora ule ule, huku akilinda nafasi yake ya kuwa kipa namba moja wa timu ya Taifa, Taifa Stars.

Pamoja na timu yake ya Azam msimu huu kutokufanya vizuri kwenye Ligi Kuu hasa mzunguko wa kwanza, lakini bado ameendelea kuwa imara kwa kuokoa michomo ya wapinzani kwa ustadi mkubwa.

4. Daniel Agyei-Simba
Angalau wanachama na mashabiki wa Simba wamekuwa watulivu mara baada ya kusajiliwa kwa kipa Mghana Daniel Agyei kwenye kipindi cha dirisha dogo.
Ni baada ya kutokuwa na imani na Vicent Angban ambaye walidai alikuwa akifungwa mabao mepesi mno.

Agyei, ameonekana kutibu tatizo hilo, ingawa kwenye mechi za karibuni amekuwa akitatizwa na kukosekana na beki Methold Mwanjale, hivyo kuruhusu nyavu zake kutingishwa, kutokana na uzembe na makosa ya mabeki wake.

Alishawahi kucheza mechi zaidi ya sita bila kuruhusu bao, wakati beki ikiwa imara chini ya Mzimbabwe Mwanjale.

Anahesabika kuwa mmoja wa makipa waliotamba msimu huu.

5.Youthe Rostand-African Lyon
Moja ya vitu ambavyo African Lyon inajivunia ni kuwa na kipa mwenye uwezo wa hali ya juu kama Youthe Rostand.

Kipa huyo raia wa Cameroon alikuwa mwiba kwa washambuliaji anaposimama langoni kwa kuokoa makombora makali, huku akiwa na staili yake ya kupoteza muda timu yake inapokuwa mbele kwa ushindi.

Urefu wake, mwili uliojengeka, umekuwa ukiongeza ugumu kufungika.

Yeyote anayemfunga ni lazima awe amefanya kazi ya ziada na si kumfunga mabao rahisi na ya kizembe.

Kabla haijaangukia kwa Agyei, Simba ilikuwa na mpango wa kumsajili kipindi cha dirisha dogo.

Lakini pia kuna taarifa kuwa Yanga huenda ikamsajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Hakika ni kipa aliyefanya vizuri sana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu inayoelekea ukingoni.
Baada ya kikosi cha Yanga kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), benchi la ufundi la timu hiyo chini ya mkufunzi wake George Lwandamina raia wa Zambia, limeweka hadharani kuwa mipango yao ni kuhakikisha kikosi hicho kinatwaa mataji mawili msimu huu; ligi kuu na Kombe la FA.

Yanga walitinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Prisons ya Mbeya kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa robo fainali uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar juzi Jumamosi.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, amesema kuwa, wanataka makombe hayo kwa ajili ya kupooza machungu waliyonayo baada ya kutolewa kwenye michuano ya kimataifa ambako walielekeza nguvu zao msimu huu.

“Nguvu kubwa ilikuwa ni kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kila kitu kiligeuka ndoto baada ya kutolewa, hivyo akili zetu ni kuhakikisha tunachukua makombe yaliyobakia hapa nyumbani.

“Tuna nafasi nzuri kwenye ligi, japo Simba wapo juu yetu kwa sasa, hilo halituogopeshi sana kwani tukishinda mechi zetu za viporo, mambo yatakuwa sawa, pia tunataka kufanya vizuri katika FA kwa ajili ya kujihakikishia nafasi ya kutinga michuano ya kimataifa msimu ujao,” alisema kocha huyo.
Hatimaye Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeipokonya pointi tatu Simba SC, ilizokuwa imepewa kutoka kwa Klabu ya Kagera Sugar.

Awali, Simba ilikuwa imepewa ushindi wa mezani wa pointi tatu na magoli matatu dhidi ya Kagera Sugar, baada ya mchezo wake na timu hiyo ya mkoani Kagera kumalizika ikiwa imepigwa magoli 2-1.

Ushindi huo wa mezani ulitokana na malalamiko kuwa Kagera Sugar ilimchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano, hivyo hakuwa na sifa za kushiriki mchezo huo kwa mujibu wa kanuni na sheria za Soka.

Akitangaza uamuzi wa kurejesha matokeo ya awali ya uwanjani leo katika ukumbi wa Habari wa TFF, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Selestin Mwesigwa alisema kuwa sababu zilizopelekea Kamati kuchukua uamuzi huo, ni pamoja na kucheleweshwa kwa malalamiko ya Simba SC dhidi ya Kagera Sugar, Simba kushindwa kulipia ada ya rufaa dhidi ya maamuzi ya mechi hiyo na kukosekana kwa uhalali wa Kamati ya Saa 72 kwa kuwahusisha wajumbe waalikwa ambao hawakuwa na sifa za kuwa kwenye kamati hiyo.

Kutokana na uamuzi huo, Simba imeendelea kuwa kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), ikiwa na pointi 59 badala ya 62 za awali.

Hali hiyo inawapa nafuu ya kupumua watani wao wa jadi, Young Africans ambao wana pointi 56 huku wakiwa na michezo miwili nyuma ya Simba FC.
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungia Haji Manara (Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba) kutojihusisha na masuala ya soka kwa mwaka mmoja na pia anatakiwa kulipa faini ya Shilingi  Milioni tisa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Jerome Msemwa amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya Manara kukutwa na makosa matatu dhidi ya TFF ambao ni walalamikaji.

Makosa hayo ya Manara dhidi ya mlalamikaji TFF ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila na la tatu kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.
 
Siku chache zilizopita  Manara aliituhumu TFF kufanya njama za waziwazi ili kuwabeba wapinzani wao Yanga kwenye Ligi Kuu.

Manara pia aliwatuhumu viongozi wakuu wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa ni wahaya na viongozi wa zamani wa Yanga, ambao wanataka kuipendelea Kagera Sugar.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta 

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta yuko mbioni kurithi mikoba ya mshambuliaji wa zamani wa Arsenal na Manchester United, Robin van Persie katika klabu ya Fenerbahce ya Uturuki.

Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji ni miongoni mwa wachezaji wanne wanaotafutwa na Fenerbahce katika dirisha lijalo la usajili, wengine ni Theo Bongonda, Ridgeciano Haps na Thomas Bruns

Uamuzi wa Fenerbahce kumtaja Samatta katika orodha yao ya usajili inaonekana kushangaza wengi barani Ulaya.

Hata hivyo, rekodi za Mtanzania huyo mwenye mkataba na Genk hadi 2020, katika msimu huu amefunga mabao 19 akitoa pasi tano za mabao katika mechi 49 alizocheza za mashindano yote hadi sasa.

Pia, hivi karibuni Samatta aliweka rekodi ya kufunga mabao matano katika mechi sita mfululizo rekodi inayoonyesha kuivutia zaidi Fenerbahce inayotaka kutengeneza kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Uturuki na mashindano ya Ulaya.

Kwa  mujibu mtandao wa fotospor, Meneja Utawala wa Fenerbahce, Hassan Cetinkaya alikuwepo uwanjani kwenye mchezo wa kwanza wa Europa Ligi kati ya Celta Vigo na Genk kwa ajili ya kumtazama Samatta pamoja na mchezaji wa Celta Vigo, Theo Bongonda.

Kuingia kwa Samatta katika rada za Fenerbahce ni wazi siku za mkongwe Van Persie aliyebakiza miaka miwili zimeanza kuhesabika hasa baada ya kupungua kwa kasi yake ya kuzifumania nyavu msimu huu. Van Persie amefunga mabao sita katika mechi 25 alizoichezea Fenerbahce katika mashindano mbalimbali msimu huu.

Mbali ya Waturuki hao Samatta tayari ameanza kuzivutia timu za Ligi Kuu England pamoja na Ujerumani zinadaiwa kuwania saini yake mwisho wa msimu huu.

Klabu tatu za Ujerumani zinazoshiriki Bundesliga ni Wolsfburg,  Hamburger SV na Borussia Moenchengladbach zimeonyesha nia ya wazi ya kutaka huduma ya Samatta.

Iwapo Samatta atafanikiwa kujiunga na Fenerbahce atakuwa pamoja na nyota kama Gregory Van Der Wiel, Raul Meirelles, Miroslav Stoch, Martin Skrtel, Emannuel Emenike, Simon Kjaer, Moussa Sow na Mehmet Topal huku wakifundishwa na kocha Dick Advocaat kutoka Uholanzi.
Mfungaji wa bao la kwanza la Manchester United, Marcus Rashford dakika ya saba tu katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Chelsea kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England Uwanja wa Old Trafford akishangilia baada ya kumpa raha kocha wake, Jose Mourinho. Bao la pili la United limefungwa na Ander Herrera dakika ya 49. Pamoja na kufungwa Chelsea inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 75 za mechi 32 wakati United pia inaendelea kushika nafasi ya tano kwa pointi zake 60 za mechi 31

Roberto Firmino alifunga bao la ushindi na kuiwezesha Liverpool kupanda hadi nafasi ya tatu katika jedwali la Primia Ligi

Mshambualia huyo mbrazil alifungia Liverpool mwisho mwisho ya kipindi cha kwanza.

Milner alifanya madhambi kipindi cha pilia lakiki Simon Mignolet, akafanikiwa kuukoa bao kutokana na mkwaju kutoka kwa Matt Phillips.

Baadaye Alberto Moreno akakosa la wazi baada ya kipa wa Albion Ben Foster kuruka kukoa kona.

Licha ya kukosa bao hilo kikosi cha Jurgen Klopp kilipata ushindi wa tatu katika mechi saba huku West Brom wakipata kipigo mara tatu mfululizo.
Timu ya Taifa ya vijana wa chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) imepata nafuu zaidi kuelekea kufuzu mashindano ya Kombe la Dunia nchini India baada ya hatua ya Shirikisho la Kandanda Duniani (Fifa) kuifungia Mali kushiriki katika mashindano ya fainali za Afrika kwa Vijana nchini Gabon.

Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema kuwa tayari Shirikisho la Kandanda la Afrika (Caf) limeindoa Mali imeitangaza nchi ya Ethiopia kuungana na Tanzania, Angola na Niger katika kundi B la mashindano hayo.

Lucas amesema kuwa Mali ndiyo mabingwa watetezi wa mashindano hayo na walikuwa  na kikosi chenye wachezaji nyota ambao kwa namna moja au nyingine wangeisumbua sana Serengeti Boys.

Wakati huo huo: timu ya Serengeti Boys itacheza mechi tatu za kirafiki nchini Morocco ikiwa ni sehemu ya maandalizi kabla ya kwenda Cameroon na Gabon.

Timu hiyo itacheze mechi mbili dhidi ya Gabon siku ya Aprili 22 na 25 na baadaye itacheza mechi dhidi ya Morocco  Aprili 28 na baadaye kusafiri kwenda  Cameroon kucheza mechi mbili dhidi ya Cameroon Mei 3 na Mei 6 na seku inayofuata timu itasafiri kwenda Gabon.