SIMBA SC YAWANIA TAJI LA 40 LEO
Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
TIMU
ya soka ya Simba SC, leo inawania taji la 40 tangu ianzishwe mwaka
1936, wakati itakapomenyana na KCC ya Uganda katika Fainali ya Kombe la
Mapinduzi, Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Timu
hiyo maarufu kama Wekundu wa Msimbazi, ilianzishwa mwaka 1936, enzi
hizo ikijulikana kwa jina la Queens, yaani Watoto wa Malkia, kabla ya
baadaye kubadilisha jina na kuwa Eagles, yaani ndege aina ya Tai, jina
ambalo halikudumu sana nalo likatupwa na kuwa Sunderland, ambalo
lilidumu hadi mwaka 1971 lilipobadilishwa na kuwa Simba SC hadi leo.
Kikosi kazi; Kikosi cha Simba SC katika Kombe la Mapinduzi |
MATAJI YA SIMBA SC
UBINGWA WA LIGI KUU:
1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004 na 2007 (Ligi Ndogo), 2010 na 2012.
KOMBE LA NYERERE:
1984, 1995 na 2000
KOMBE LA MUUNGANO:
1993, 1994, 1995, 2001, na 2002
KOMBE LA TUSKER:
2001, 2002, 2003 na 2005
KOMBE LA KAGAME:
1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002
KOMBE LA MAPINDUZI:
2008 na 2011
KOMBE LA MTANI JEMBE:
2013:
Sababu
ya kuachana na jina la Sunderland ni aliyekuwa Rais wa Kwanza wa
Zanzibar, Abeid Amaan Karume (sasa marehemu), ambaye wakati anaweka jiwe
la msingi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la klabu hiyo, lililopo Mtaa wa
Msimbazi, mwaka 1971, alikemea tabia ya kupenda kuiga mambo ya
Waingereza, akiamini kufanya hivyo ni kuendelea kuutukuza ukoloni.
Rais
Karume, aliwaambia Simba waachane na majina ya kizungu na watumie jina
la asili ya Afrika na ndipo jina la Mnyama tishio zaidi porini, Mfalme
wa Nyika, Simba, lilipowavutia hata ukawa mwanzo wa Simba SC tishio hii
ya leo, inayomtesa mtani wake, Yanga SC.
Katika
kipindi chote cha uhai wa klabu hiyo, imetwaa Kombe la ubingwa wa Ligi
Kuu ya Bara mara 18, Kombe la Nyerere mara tatu, Muungano mara tano,
Tusker mara nne, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama
Kombe la Kagame mara sita, Nani Mtani Jembe mara moja na Mapinduzi mara
mbili, hayo yakiwa ni jumla ya mataji 39.
Leo
Wekundu wa Msimbazi wanataka kuweka rekodi ya kutimiza mataji 40 Uwanja
wa Amaan, mbele ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, mchezo
utakaoanza Saa 10:00 jioni.
Kikosi cha KCC ya Uganda kilichowavua ubingwa Azam FC |
WANAOWANIA UFUNGAJI BORA KOMBE LA MAPINDUZI
Owen Kasuule URA 4
Amri Kiemba Simba SC 3
Feni Ali URA 3
Rama Singano Simba SC 2
Tony Odur KCC 2
Brian Umony Azam FC 2
Jose Kimwaga Azam FC 2
M. Mngwali Chuoni 2
H. Waswa KCC 2
Mechi
ya leo inazikutanisha kwa mara ya pili Simba SC na KCC, timu ya Mamlaka
ya Jiji la Kampala, baada ya awali pia kukutana katika mchezo wa Kundi B
na kutoka sare ya bila kufungana.
Kocha
wa Simba SC, Zdravko Logarusic amesema kwamba amewaandaa vyema vijana
wake kuelekea mchezo wa leo na watapigana kufa na kupona dhidi ya timu
bora ya Uganda ili kupata matokeo mazuri leo.
“Itakuwa
mechi ngumu sana, hii ni fainali. Wazi ni mechi tofauti sana na zile
zilizotangulia, unacheza unaliona Kombe na unataka kulibeba,
nimezungumza sana na vijana wangu, naamini hawataniangusha,”alisema
Logarusic raia wa Croatia, ambaye mwezi uliopita aliipa Simba taji la
kwanza, Mtani Jembe kwa kuwafunga watani, Yanga 3-1.
Kipa
wa Simba SC, Ivon Philip Mapunda ‘Ivo’ amedaka mechi nne za mashindano
haya bila kufungwa hata bao moja na bila shaka leo atataka kumaliza
michuano bila kumbukumbu ya kuokota mpira nyavuni ili pia kujitengenezea
mazingira ya kuwa kipa bora wa Kombe la Mapinduzi 2014.
Kiungo
Amri Ramadhani Kiemba amefunga mabao matatu hadi sasa kwenye mashindano
haya, anazidiwa bao moja tu na mchezaji anayeongoza, Owen Kasuule wa
URA ya Uganda iliyotolewa na Simba SC katika Nusu Fainali.
Ramadhani
Yahya Singano ‘Messi’ amecheza vizuri katika mechi zote nne alizopangwa
na hadi sasa ni kati ya wachezaji wanaotazamiwa kutwaa tuzo ya mchezaji
bora wa mashindano.
Wachezaji
hawa watatu, Mapunda, Kiemba na Messi hakika leo wanatarajiwa kuwa
chachu ya matokeo mazuri kwa Simba SC- mbele ya KCC yenye matumaini
makubwa ya kuondoka na Kombe la Mapinduzi.
Kampuni
ya CXC Safaris & Tours ya Dar es Salaam, chini ya Mkurugenzi wake,
Charles Hamkah inatarajiwa kutoa Sh. 300,000 kwa kila mmoja, mfungaji
bora, mchezaji bora na kipa bora.
Hii
ni michuano ya nane ya Kombe la Mapinduzi inayokuja sambamba na sherehe
za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu kung’olewa kwa utawala
dhalimu wa kisultani visiwani hapa.
Timu
tano zimetwaa Kombe hilo tangu limeanzishwa mwaka 2007, Yanga SC ya Dar
es Salaam ikikata utepe, ikifuatiwa na watani wao, Simba SC (2008),
Miembeni ya hapa (2009), Mtibwa Sugar ya Morogoro (2010), Simba SC tena
2011 na Azam FC mara mbili mfululizo 2012 na 2013.
Mabingwa
watetezi, Azam safari hii wamekwama kwenye Nusu Fainali baada ya
kutolewa na KCC kwa kufungwa mabao 3-2, ikitoka nyuma kwa 2-0.
Kocha Logarusic mbele wakati wanapokea Kombe la Nani Mtani Jembe Desemba 21 |
Katika
mchezo wa leo, unaotarajiwa kuchezeshwa na refa mwenye beji ya FIFA,
Ramadhani Ibada ‘Kibo’, vikosi vya timu zote vinatarajiwa kuwa;
Simba
SC; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Donald Mosoti
‘Beki Adui’, Joseph Owino, Jonas Mkude, Haroun Chanongo, Amri Kiemba,
Amisi Tmbwe, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Awadh Juma.
KCC;
Omar Magoola, Saka Mpima, Habib Kavuma, Ibrahim Kiiza, Fahad Kawooya,
Gadafi Kiwanuka, Herman Wasswa, Tom Masiko, Tony Odur, Stephen Bengo na
William Wadri.
Category: tanzania
0 comments