JULIO: KUFUKUZWA SIMBA NA KING WANGU KUMENIFANYA NIUCHUKIE MPIRA…LAKINI AZAM FC NAWATAMANI SANA!!
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
BAADA
ya kufukuzwa kazi na klabu ya Simba SC, aliyekuwa kocha msaidizi wa
timu hiyo, Jamhuri Kiwhelo `Julio` amesema kitendo hicho kimemfanya
auchukiae mpira wa Tanzania kwa sasa.
Julio alisema wapo watu wanasababisha mambo haya kutokea. Si Rage hata kidogo bali kuna watu wanafanya umafia huu.
“Mimi
simtetei Rage, hata haya mambo ya Okwi wapo wanaosababisha na si
mwenyekiti. Mimi na King Kibadeni tumefukuzwa bila sababu. Hawakuwa na
sababu yoyote ile. Njia anazoenda nazo Rage zinaweza kuleta tija kwa
soka la klabu, tofauti na mawazo ya watu”. Alisema Julio.
Julio
aliendelea kueleza kuwa huwezi kumfukuza kocha kwasababu timu iko
nafasi ya nne katika msimamo wa ligi baada ya mzunguko wa kwanza
kumalizika.
“Ingekuwa
kocha anafukuzwa kwasababu hiyo, angefukuzwa David Moyes ambaye timu
yake ni ya tisa. Man United kuna watu wenye akili na pesa, lakini hawana
mpango wa kumfukuza”. Alisema Julio.
Kocha
huyo mwenye historian na Simba alisisitiza kuwa mpira wa Tanzania
unaendeshwa kinafiki na fitina, hivyo kufika mbali ni kuota mchana
kweupe.
Aidha Julio alikiri kuwa kwa sasa Azam fc ndio klabu bora kuanzia mfumo wa uendeshaji wa klabu pamoja na soka la vijana.
“Mimi
Julio naipenda Simba sc, lakini ukiniuliza ni timu gani napenda
kufundisha, nitakwambia ni Azam fc. Wanajali, wana misingi bora ya
Uongozi na wana mipango mizuri sana ya soka la vijana, wanalipa fedha
nzuri na ndio maana wanafanikiwa kuliko timu za Simba na Yanga zenye
fitina nyingi”. Aliongeza Julio.
Pia
kocha huyo alisisitiza kuwa timu za Simba na Yanga si mikono salama kwa
makocha na wachezaji wa Tanzania kwasababu hazina mfumo maalumu wa
kuendeleza soka la vijana na huwa zina maamuzi ya haraka kufukuza
makocha.
“Wachezaji
wetu wanakimbilia timu hizo kwa madai ya kutaka kufahamika na kupata
fedha nyingi. Watafika pale, lakini hawatafika wanapohitaji kwani kuna
mambo ya ajabu katika klabu hizi. Si mikono salama hata kidogo”. Alisema
Julio.
Julio
aliunga mkono Jitihada za rais wa TFF, Jamal Malinzi kutaka timu ya
Taifa ya Tanzania, Taifa stars icheze fainali za mataifa ya Afrika 2015,
lakini akakiri ugumu kwasababu hakuna mfumo mzuri.
“Hatuna
shule za soka, mfumo mbaya wa uendesheji wa soka la vijana, mfano
michuano ya copa coca cola, Uhai Cup inakuja kwa muda mfupi. Kwa msingi
huu hatuwezi kufika sehemu yote”. Alisema Julio.
Category: tanzania
0 comments