Yanga yaendeleza rekodi Ligi Kuu
WAKATI jumla ya mabao 19 yamefungwa kwenye mechi za raundi ya kwanza ya ligi hiyo iliyoanza juzi na kuendelea jana, Yanga imeendeleza rekodi ya Ligi Kuu Bara baada ya kulazimisha sare dhidi ya vijana wa Suleiman Matola, Lipuli FC ya Iringa.
Tangu msimu wa 2010/11, haijawahi kutokea mechi za ufunguzi za ligi hiyo kuchezwa bila kuwapo na mechi hata moja yenye matokeo ya sare, jambo ambalo kama mechi hiyo ya jana timu mojawapo ingeshinda basi ingekuwa ni rekodi mpya.
Aidha, mabao 19 yaliyofungwa katika mechi za ufunguzi msimu huu yamevunja rekodi ya magoli yaliyofungwa katika mechi za ufunguzi msimu uliopita uliokuwa na mabao 12 kwenye mechi zake za raundi ya kwanza.
Idadi hiyo ya mabao imepatikana baada ya matokeo ya Simba kushinda 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, Mwadui kuifunga Singida United 2-1 na Prisons kuitandika Njombe Mji 2-1.
Matokeo mengine ni Azam kuifunga Ndanda bao 1-0, Mbeya City kushinda bao 1-0 dhidi ya Majimaji, Mbao kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, Mtibwa kuifunga Stand United 1-0 kabla ya jana Yanga kulazimishwa sare ya bao moja kwa moja.
Katika mechi ya jana ambayo ilipigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Yanga ambao walikuwa wanatafuta ushindi hasa baada ya watani zao wa jadi, Simba kuanza kwa kishindo cha ushindi wa bao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, jana walikosa maarifa ya kuipenya ngome ya Lipuli iliyokuwa chini ya Asante Kwasi, aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Mbao FC.
Wageni, Lipuli ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 44 kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Azam FC na JKT Ruvu, Seif Abdallah, aliyepiga shuti upande wa kulia wa Uwanja lililoenda moja kwa moja nyavuni na kumshinda golikipa Youthi Rostand.
Bao hilo lilidumu kwa dakika moja tu kutokana na Thaban Kamusoko kuisawazishia timu yake kwa kichwa akiunganisha nyavuni mpira wa kona uliochongwa na Ibrahim Ajibu.
Baada ya bao hilo, liliwafanya wachezaji wa Lipuli kumzinga mwamuzi Hans Mabena kufuatia mpira uliopigwa na Kamusoko kugonga mwamba wa juu na kuangukia ndani huku wachezaji wakidhani mpira huo uliangukia nje ya goli.
Pamoja na Yanga kufanya mashambulizi mfululizo, Lipuli walikuwa imara na kufanikiwa kuwabana Yanga wasipate bao la pili.
Hata hivyo, Lipuli ilipata pigo baada ya beki wake Kwasi kupewa kadi ya pili ya njano iliyomfanya kutolewa kwa nyekundu zikiwa zimebaki dakika mbili mpira kumalizika.
Baada ya mpira kumalizika mashabiki wa Yanga walionekana kuwatolea maneno machafu wachezaji wa Lipuli huku wakiwatuhumu kwa vitendo vyao vya kujiangusha mwishoni mwa kipindi cha pili.
Katika mchezo huo kiungo wa Yanga, Kabamba Tshishimbi alishindwa kuonyesha makeke yake kama alivyofanya kwenye mchezo dhidi ya Simba baada ya kubanwa na viungo wa Lipuli Sahaban Zuberi na Mussa Nampaka.
Category: tanzania
0 comments