Hii ndio orodha ya Mabeki 10 ghali zaidi duniani

Unknown | 12:36 PM | 0 comments

KYLE WALKER

HATUA ya Tottenham kukamilisha usajili wa beki Davinson Sanchez, kumemfanya mlinzi huyo kuwa ingizo jipya katika orodha ya mabeki 10 ghali zaidi duniani.

Sanchez amejiunga na Tottenham akitokea Ajax ya Uholanzi huku pia licha ya kuingia katika orodha ya mabeki 10 ghali zaidi duniani, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kununuliwa katika historia ya klabu hiyo.

Kadhalika, Sanchez, 21, ndiye mchezaji kinda zaidi katika orodha hii ya mabeki 10 ghali zaidi, ambao nane kati ya hao ni uhamisho unaozihusisha klabu za Premier League na wanne wao wakiihusisha Manchester City.

Pia kutua huko kwa Sanchez Spurs, kunafanya mabeki watano kati ya hao 10 ghali, usajili wao umefanyika majira haya ya joto, wakati huu dirisha hilo likiendelea barani Ulaya kabla ya kufungwa Alhamisi saa sita usiku wiki hii.

Hapa ni mabeki hao10 ghali zaidi na kiasi cha fedha kilichotumika kuwanunua, je wana thamani hiyo?...

BENJAMIN MENDY – Monaco kwenda Man City (pauni milioni 51.75)

Pep Guardiola alivunja rekodi wakati alipomsajili Mendy kutoka Monaco Julai 24, mwaka huu, beki huyo wa kushoto ambaye ndiye ghali zaidi Ulaya, haraka alipata mafanikio msimu wa 2016-17 kwa kutwaa ubingwa wa Ligue 1 na kufika nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu yake hiyo ya awali.

Kutua kwake ni moja ya mkakati wa kutaka kushangaza kwa beki ya Man City, ambao umeifanya kutumia pauni milioni 165 kwa kununua mabeki watatu na kipa Ederson.

DAVID LUIZ – Chelsea kwenda PSG, pauni milioni 50

Dau hilo la Mendy, limefunika pauni milioni 50 Paris Saint-Germain ilizolipa wakati ikimsajili beki huyo wa kimataifa wa Brazil, Luiz kutoka Chelsea mwaka 2014.

Luiz alitwaa ubingwa wa Ligue 1 kwa misimu yote aliyoichezea PSG na amefanya hivyo mara tatu mfululizo huku akirudi Chelsea kwa pauni milioni 34 katika uhamisho wa kushangaza Agosti 2016, na kutwaa medali kwa kushinda Premier League.

KYLE WALKER – Tottenham kwenda Man City, pauni milioni 50

Wakati Walker anajiunga na Spurs akitokea klabu ya nyumbani kwao Sheffield United kwa pauni milioni tano mwaka 2009, mambo machache yalidhaniwa ikiwa ni pamoja na siku moja anaweza kuwa mchezaji ghali zaidi England.

Majumuisho hayo yote yanamaanisha Walker – ambaye hajawahi kutwaa kombe lolote katika wasifu wake kisoka– ana ‘chata’ kubwa ya kuweza kuishi Uwanja wa Etihad.

JOHN STONES – Everton kwenda Man City, pauni milioni 47.5

City ilionyesha kuridhika kulipa kiasi hicho kikubwa kwa kipaji hiki cha England, wakati Stones akijiunga na klabu hiyo kutoka Everton mwaka jana.

Lakini Stones, 23, alikumbwa na wakati mgumu katika mwaka wa kwanza wa Guardiola kwenye kikosi hicho kwa kucheza chini ya kiwango, wakiruhusu mabao mengi huku wakimaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi. Hata hivyo, kwa uwezo wa Stones unaweza bado kumuona akiendeleza kipaji chake.

DAVINSON SANCHEZ – Ajax kwenda Tottenham, pauni milioni 36.6

Spurs ilisubiri kwa wiki kadhaa kukamilisha usajili wao wa kwanza majira haya ya joto, lakini ikafanya hivyo staili yake, kwa kuvunja rekodi ya usajili wao na kumleta Sanchez Kaskazini mwa London.

Beki huyo wa zamani wa Atletico Nacional, aliripotiwa kuwa katika rada za Barcelona wakati Ajax ikitinga hatua ya fainali ya michuano ya Europa League mwaka jana, lakini baada kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Manchester United, Jose Mourinho alifichua hofu ya uwezo wa mchezaji huyo ya kuwa na mpira miguuni mwake.

LEONARDO BONUCCI – Juventus kwenda AC Milan, pauni milioni 35.2

Kocha wa Juve, Massimiliano Allegri, alimshuhudia Bonucci akiruhusiwa kujiunga na wapinzani wao wa Serie A, AC Milan, ambayo ilimwaga fedha za kutosha sokoni ili kuweza kurudi Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Bonucci alitwaa ubingwa wa Serie A mara sita akiwa Juventus, lakini mara mbili walipoteza mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kusajiliwa kwa beki huyo wa kimataifa wa Italia– aliyeripotiwa kuwindwa na Chelsea –kulifanya mapinduzi makubwa kwa Milan.

SHKODRAN MUSTAFI – Valencia kwenda Arsenal, pauni milioni 35

Arsenal kawaida haijulikani kwa kutumia kiasi kikubwa kununua, huku kocha Arsene Wenger akijulikana katika ulimwengu wa soka kwa ubahili, lakini alitoa pauni milioni na kumsajili Mustafi kutoka Valencia Agosti 2016.

Beki huyo wa kimataifa wa Ujerumani alikuwa kisiki katika msimu wake wa kwanza Uwanja wa Emirates, lakini 'Gunners' ilikosa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa mara ya kwanza tangu 1997.

ANTONIO RUDIGER – Roma kwenda Chelsea, pauni milioni 34

Wakati nguli wa klabu, John Terry, akiwa ameondoka Stamford Bridge, Chelsea ilikuwa katika mahitaji ya kusaka beki mpya wa kumrithi na ilimgeukia mshiriki mwenza wa Mustafi kimataifa kikazi, Rudiger, ambaye alijiunga nayo akitokea Roma.

Rudiger, 24, alitua London akiwa ndiyo kwanza wa moto akitokea kuipa mafanikio Ujerumani kwa kuibebesha Kombe la Mabara.

THIAGO SILVA – Milan kwenda PSG, pauni milioni 33

Ingizo la pili la PSG ni nahodha wa klabu yao, Thiago Silva, kwani Mbrazil huyo amekuwa chanzo cha mafanikio makubwa tangu alipojiunga nayo mwaka 2012.

Ingawa PSG ilikuwa imesimamishwa na Monaco kwa kukomesha utawala wao wa Ligue 1 msimu uliopita, Silva (32), ameiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligue 1 mara nne na mara tatu wa Coupes de France.

ELIAQUIM MANGALA – Porto kwenda Man City, pauni milioni 32

Anguko kubwa la ada ya uhamisho wakati Mangala akijiunga na City kwa pauni milioni 32 kutoka Porto, lilionekana kuongezeka vya kutosha baada ya kuruhusiwa kujiunga na Valencia kwa mkopo. Lakini nyaraka zilizovuja baadaye zilipendekeza gharama ya jumla ya Mangala iliongezeka hadi pauni milioni 42.

Mangala alitarajiwa kuruhusiwa kuondoka na kocha Pep Guardiola, amecheza mechi 48 Premier League.

(*Gharama hizi zimeripotiwa kwa muda mara baada ya usajili kukamilika.)

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments