TIMU ZA COMORO HUWA ‘HAZIPINDUI’ KWA YANGA, WANA JANGWANI LEO RAHA TU TAIFA

Unknown | 7:25 AM | 0 comments




Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga SC ya Dar es Salaam leo wanaanza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kumenyana na Komorozine ya Comoro katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amesema wachezaji wake waliopo kambini Bagamoyo wapo 'fiti' kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza Saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wenye uwezo wa kubeba watu wapatao 60,000.
Pluijm ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba maandalizi ya mchezo huo kwa kikosi chake yamekamilika na vijana wote wako fiti, kiakili na morali yao iko juu hivyo anaamini wataibuka na ushindi.
“Nimekuwa na timu kwa takribani wiki nne sasa tangu niungane na wachezaji nchini Uturuki, maendeleo ni mazuri, upungufu uliojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City tumeufanyia kazi na sasa kikosi kimezidi kuimarika,”alisema.





Kikosi cha ushindi: Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuendelea kuwa hivi hivi leo, waliosimama kutoka kulia ni Frank Domayo, Kevin Yondan, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Didier Kavumbangu na kipa Deo Munishi, wakati walioinama kutoka kulia ni David Luhende, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Mrisho Ngassa. Kuna uwezekano Hamisi Kiiza akachukua nafasi ya Simon Msuva.

Kihistoria, timu za Comoro zimekuwa hazifurukuti kwa Yanga SC na Komorozine inakuwa timu ya tatu kukutana na timu hiyo ya Jangwani kwenye michuano ya Afrika baada ya AJSM na Etoile d'Or Mirontsy.
Januari 27, mwaka 2007 katika Ligi ya Mabingwa Afrika Raundi ya Awali Yanga iliifunga AJSM mabao 5-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na moja kwa moja kufuzu Raundi ya Kwanza, kwa sababu hakukuwa na mchezo wa marudiano kwa kuwa Comoro hawakuwa na Uwanja wenye kukidhi sifa za michuano ya Afrika.
Hiyo ilikuwa mara ya mwisho Yanga SC kufika mbali kidogo kwenye michuano hiyo, ikiwa chini ya kocha Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’, kwani katika Raundi ya Kwanza pia iliitoa timu ngumu Petro Atletico ya Angola kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 3-0 nyumbani na kwenda kufungwa 2-0 ugenini. 
Hata hivyo, kasi za Yanga ziliishia mbele ya Esperance ya Tunisia baada ya kutolewa kwa jumla ya mabao 3-0 katika hatua ya 16 bora, iliyofungiwa ugenini yote kabla ya kuja kulazimisha sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. 
Kwa matokeo hayo, Yanga iliingia kwenye kapu la kuwania kucheza Kombe la Shirikisho na kutolewa na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0, iliyofungiwa ugenini katika mchezo wa marudiano baada ya sare ya 0-0 mjini Mwanza katika mchezo ambao Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji (kabla hajawa Mwenyekiti, akiwa mfadhili tu) alitoa Sh. Milioni 100 mashabiki waingie bure.
Mwaka 2009, Yanga iliitoa timu nyingine ya Comoro, Etoile de Mironsty kwa jumla ya mabao 14-1, ikianza kushinda 8-1 Januari 31 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kushinda 6-0 ugenini, wakati huo ikiwa chini ya kocha mwingine Mserbia, Profesa Dusan Savo Kondic.
Kwa mara nyingine mbio za Yanga ziliishia mbele ya timu ya Kaskazini mwa Afrika, baada ya kutolewa na mabingwa wa kihistoria Afrika, Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 4-0, ikianza kufungwa 3-0 Machi 15 mjini Cairo  na baadaye 1-0 Dar es Salaam.
Mechi ya Cairo alidaka kipa Mserbia, Obren Curkovick na Dar es Salaam alidaka Juma Kaseja.
Yanga ambayo ilikuwa kambini Bagamoyo kujiandaa na mchezo wa leo, ikifanya mazoezi mara mbili kwa siku, wakifanikiwa kuwatoa Wacomoro hao baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini ndani ya wiki mbili, watakutana tena na Ahly , ambao ndio mabingwa wa Afrika.
Vijana wapo tayari; Kocha wa Yanga Hans van der Pluijm amesema vijana wake tayari





REKODI YA YANGA NA TIMU COMORO



MWAKA 2007: 
Januari 27, 2007;  Yanga 5-1 AJSM 
(Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika, hakukuwa na mechi ya marudiano, Yanga ilifuzu)

MWAKA 2009:
Januari 31; Yanga 8-1 Etoile d'Or Mirontsy
Februari 13; Etoile d'Or Mirontsy 0-6 Yanga

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments