MANDELA ALIVYOITUMIA MICHEZO KULETA UMOJA, ANGALIA SIKU ALIVYOKUTANA NA WATANZANIA NA KUWAFANANISHA NA JAMAICA
MANDELA AKIWA NA TIMU YA OLIMPIKI YA TANZANIA MWAKA 2000 MJINI SYDNEY, AUSTRALIA |
Na Saleh Ally
“Jela si kuwa inachukua uhuru wako pekee,
badala yake inachukua hata utambulisho wako wa wewe ni nani kwa kuwa kila mmoja
anavaa sare, anakula chakula sawa na wengine na anafuata ratiba zilezile.
“Kwa kifupi ni wizi wa uhuru wa mhusika
na kama mpigania uhuru na mwanaume wa shoka, kikubwa ni kupambana kwa nguvu
zote na hali hiyo ambayo inaua au kupoteza muonekano wa uwezo wa watu husika.”
Maneno hayo yako mwanzo kabisa
kinapoanza kitabu cha Long Walk To Freedom Volume 2 cha Nelson Mandela ambacho
nilikinunua Mei 24, 2003 kwenye nyumba ya makumbusho ya Mandela iliyoko katika Mtaa
wa Villakazi, Soweto jijini Johannesburg.
Ni miaka kumi na ushee sasa tangu wakati
huo, tukiwa na watu wengine wachache tulipata kuonyeshwa vyombo, nguo, viatu na
vitu vingine alivyokuwa akivitumia Mandela wakati akiishi katika nyumba hiyo na
mkewe, Winnie Mandela.
Baadaye tukatembezwa kwenye nyumba
ambayo alihamia Mandela na ile aliyokuwa akiishi mkewe wa zamani, Winnie
Mandela. Pamoja na mengi makubwa aliyofanya Mandela, kwangu kilichonivutia
zaidi kwake ni namna alivyoshiriki michezo.
Huenda wengi wameelezea, lakini
ukiangalia picha zake zilizokuwa katika nyumba hiyo ya makumbusho zinaonyesha
alikuwa ni mwanamichezo wa kweli, kwani si ngumi tu, mchezo uliojulikana kuwa
kipenzi chake, lakini soka na kikapu pia alishiriki.
Kwangu naamini wanaoshiriki michezo
wanaaminika kuwa binadamu wenye maamuzi ya haraka zaidi kuliko wengine, angalia
mpira wa kikapu, soka na hata ngumi namna mtu mmoja ambavyo huamua vitu vingi
kwa wakati mmoja kwa kuwa muda ni mchache na mambo mengi hutakiwa kufanyika
katika kipindi kifupi.
Kwa Mandela hakuwa Mzungu, inaonekana
imekuwa ni vigumu kwa Wazungu kutamka kuwa ndiye binadamu maarufu zaidi kuliko
wengine wote duniani katika kipindi hiki.
Kifo chake, bado kinamfanya awe
mwanasiasa maarufu zaidi kuliko wengine wote duniani, hasa aliyeshiriki katika
kupigania uhuru wa nchi fulani kwa muda mrefu zaidi na kusaidia kuiokoa nchi.
Baada ya kuwa rais mweusi wa kwanza wa
Afrika Kusini, Mandela amekuwa ndiye kiongozi mwanasiasa maarufu zaidi na
kipenzi cha wanamichezo kuliko wengine wote duniani.
Makocha maarufu, akiwemo Alex Ferguson,
amewahi kueleza namna alivyofurahishwa na maisha au ushujaa wa Mandela,
alimtembelea na kuonyesha furaha yake kwake wakati Manchester United ilipokuwa
Afrika Kusini kwa mechi za kirafiki.
Tanzania:
Kuna mengi yanayoonyesha kuwa Mandela
alikuwa na urafiki mkubwa na Tanzania, kwani hata alipokamatwa Agosti 5, 1962
na baadaye kuhukumiwa gerezani, inaelezwa alikuwa anatokea hapa nchini.
Lakini kwenye kitabu chake cha Long Walk
To Freedom, kuna maneno kadhaa ya Kiswahili yaliyotumika, ikionyesha wazi namna
alivyokuwa na mapenzi na nchi hii.
Moja ya picha kwenye kurasa hizi
zinamuonyesha akiwa na timu ya taifa ya Olimpiki ya Tanzania ambayo alipiga nayo
picha mwaka 2000.
Kiswahili:
Pamoja na kutumia Lugha ya Kiswahili
katika sehemu mbalimbali, Mandela amewahi kuonyesha ujuzi wake wa kuzungumza
lugha hiyo alipokutana na timu ya Olimpiki ya Tanzania ambayo awali aliifananisha
na Jamaica.
Daktari Mwanandi Juma Mwankemwa, ambaye
sasa ni daktari wa Azam FC, aliyekuwa kwenye timu hiyo, anasimulia namna
Mandela alivyozungumza nao kwa Lugha ya Kiswahili:
“Ilikuwa mwaka 2000 katika Michezo ya
Olimpiki kule Sydney, Australia. Siku hiyo Mandela alikuwa anapewa digrii ya
heshima katika chuo kimoja katika mji huo. Sisi tulikuwa kati ya wanamichezo
tulioteuliwa kupanga mstari kumsalimia.
“Alipotoka baada ya kuona ‘trak suti’
zetu, akatuuliza kama sisi ni timu ya taifa ya Jamaica, tulipomuambia ni
Tanzania, akaonyesha kufurahi sana, mara moja akabadili lugha na kuanza
kuzungumza Kiswahili akisema maneno haya, namnukuu.
“Watanzania rafiki zangu, wiki iliyopita
nilikuwa Arusha na rais wenu Mkapa, tulikuwa na mkutano. Hamjambo kabisa ndugu
zangu, sogeeni tupige picha.
“Baada ya hapo tulipiga naye picha
tukiwa kati ya watu wachache tuliopata nafasi hiyo ya upendeleo ambayo aliitoa
yeye binafsi. Leo ninaona kweli ilikuwa bahati kwangu na wenzangu kama Selemani
Nyambui na marehemu Erasto Zambia kwa kuwa tulipata picha na Mandela,” anasema
Mwankemwa.
Ngumi:
Katika kitabu chake cha Long Walk To
Freedom, Mandela anaelezea namna ambavyo hakuwa na mapenzi na mchezo wa ngumi,
hasa lilipofikia suala la kuumizana.
Anasema pamoja na wengi kuamini alikuwa
akiupenda sana, lakini yeye alivutiwa na baadhi tu ya sehemu kama namna mtu
anavyojipanga kujilinda na anavyocheza ulingoni kumhadaa adui.
Hata baada ya kuingia kwenye siasa rasmi
na kuamua kupambana kwa ajili ya uhuru wa Afrika Kusini, Mandela hakutaka
kuendelea na mchezo huo kabisa, ndiyo maana hakufika mbali pamoja na kudaiwa alikuwa
na kipaji cha juu katika mchezo huo. Imekuwa ikielezwa, alipenda soka zaidi.
Liverpool:
Mandela alikuwa ni shabiki mkubwa wa
Liverpool, mtu wa kwanza kutangaza hilo alikuwa ni John Barnes, winga wa zamani
mwenye kasi wa timu hiyo kigogo England.
Mwaka 1994 akiwa tayari rais wa kwanza
mweusi wa Afrika Kusini, Liverpool ilitembelea nchini humo na Mandela akapata
nafasi ya kukutana na wachezaji wa kikosi hicho, Barnes akamkabidhi jezi, naye
akaivaa.
Baadaye alipata nafasi ya kuzungumza
naye kwa saa tatu na mwisho Mandela alimtamkia kwamba yeye ni shabiki wa
Liverpool.
Katika mahojiano na FA mwaka 2003,
Barnes alisema: “Tangu nikiwa mtoto, sikuwa na tabia ya kutaka kupata sahihi za
wachezaji maarufu kama wenzangu walivyokuwa wakifanya. Lakini ilikuwa tofauti
nilipokutana na Mandela, sikujivunga hata kidogo.
“Hata kidogo wala siwezi kuona haya
kusema kuwa nimetundika ukutani nyumbani kwangu, picha niliyopiga na Mandela
kipindi hicho.”
Baada ya Barnes kueleza kuwa Mandela ni
shabiki wa Liverpool, picha yake akiwa na jezi ya Liverpool iliwekwa kwenye
mtandao wa “105 celebrity fans". Baada ya hapo watu kibao wali-like na
kati yao walikuwemo nyota kadhaa wa Marekani na wengine kama Dr Dre, Pope John
Paul II, Samuel L. Jackson, Halle Berry, Elvis Costello na Michael Schumacher.
Sahihi yake:
Mandela ndiye binadamu pekee ambaye
wanamichezo wengi nyota duniani walitaka kupata sahihi yake kama kumbukumbu.
Mara nyingi mashabiki wa michezo
mbalimbali wamekuwa wakililia kupata sahihi za mastaa wa timu katika michezo
wanayoihusudu, lakini mambo yalikuwa tofauti kwa Mandela.
Nyota lukuki kama David Beckham, Rio
Ferdnand, Tiger Woods, Robinho, Adebayor, Cristiano Ronaldo na wengine wengi
walimuomba kiongozi huyo awasainie kwenye kofia, fulana au jezi walizokuwa
nazo.
Maana yake, katika michezo saini maarufu
zaidi na iliyokuwa ikitafutwa zaidi ni ya Mandela kwa kuwa hata ambao saini zao
zimekuwa zikitafutwa kwa juhudi kubwa, nao wamekuwa wakiitafuta yake kwa udi na
uvumba.
Ukaribu:
Mandela ndiye kiongozi mkubwa na maarufu
zaidi duniani aliyekaribisha au kuwatembelea wanamichezo wengi zaidi kuliko
mwingine yeyote duniani.
Pamoja na kuwa na majukumu mengi,
madaktari kumtaka apumzike muda mrefu lakini Mandela alikuwa akitembelea sehemu
mbalimbali zilizowahusisha wanamichezo.
Aliwahi kuhudhuria fainali ya Kombe la
Mataifa Afrika mwaka 1996 wakati Afrika Kusini ilipolibeba kwa kuichapa
Tunisia. Aliwahi pia kuhudhuria mechi ya Liverpool aliyokuwa akiishangilia,
vilevile Arsenal na alikaribishwa na nahodha Tony Adams.
Ukiachana na hivyo, pamoja na kuwa na
umri wa zaidi ya miaka 85, aliendelea kutembelewa na wanamichezo mbalimbali
ambao walitamani kumuona kila walipofika Afrika Kusini.
Pamoja na msisitizo wa madaktari kwamba
alitakiwa kupumzika, mara zote alitoa ruhusa wanamichezo kumtembelea kila
aliposikia walitaka kufanya hivyo.
Manchester United, Manchester City na
timu ya taifa ya England wamewahi kumtembelea kiongozi huyo. Licha ya uzee kuwa
kikwazo kwake kuzungumza nao akiwa na nguvu vizuri, lakini bado alifurahi
kuwaona wakiwa pamoja naye.
Dawa:
Wakati fulani mmoja wa madaktari wa
Mandela aliwahi kueleza michezo ilikuwa ni kama sehemu ya dawa ya kiongozi huyo
kwa kuwa mara kadhaa alitaka kuangalia michezo mbalimbali, soka ukiwa wa
kwanza, ngumi na kikapu.
Kingine ni kutembelewa na wanamichezo,
kila ilipotokea akatembelewa na mchezaji, kocha au timu, baada ya kuondoka,
Mandela alionekana ni mchangamfu sana.
Daktari huyo alieleza kuwa uchangamfu
wake umekuwa ukiendelea hata angalau wiki nzima kila baada ya kupata ugeni wa
wanamichezo, hali ambayo wao walipenda kumuona akiwa nayo.
Katika moja ya vitabu vyake vya Long
Walk To Freedom, Mandela pia ameeleza namna alivyokuwa akiitumia michezo kama
sehemu ya kutafuta nguvu mpya.
Ameelezea mazoezi yalivyokuwa
yakimsaidia, lakini namna alivyoshiriki michezo kama sehemu ya kuupoza mwili
wake na pilika za siasa.
PICHA: SALEHE JEMBE
Category: tanzania
0 comments