Simba, Yanga vitani leo

Unknown | 11:21 AM | 0 comments

LEO ndio leo Uwanja wa taifa ambapo miamba miwili ya soka nchini Tanzania, Simba na Yanga zitakapoonyeshana ubabe kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Msisimko wa mchezo wa leo unatokana na namna msimamo wa ligi ulivyo ambapo timu hizi ndizo zilizopo kwenye mbio za ubingwa.

Timu hizi zinaingia Uwanjani leo huku zikikumbuka matokeo ya mchezo uliopita ambao waligawana pointi baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo uliochezwa Oktoba Mosi mwaka jana, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Amis Tambwe lakini Simba walikuja kusawazisha zikiwa zimebakia dakika tatu mchezo huo kumalizika.

Kocha wa Simba ambao walirejea juzi jijini Dar es Salaam wakitokea Zanzibar walipokwenda kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa leo, Joseph Omog, alisema jana kuwa amemaliza kazi yake na kazi imebakia kwa wachezaji wake ambao watatakiwa kuionyesha uwanjani.

"Tumekuwa kwenye maandalizi ya wiki nzima, vijana wapo tayari kwa mchezo huu, tutacheza soka letu la kila siku huku lengo likiwa ni ushindi tu," alisema Omog.

Alisema amefurahishwa kuona wachezaji wake wote wapo kwenye hali nzuri kitu kinachomfanya kuwa na wigo mpana wa kupanga kikosi chake.

"Siwezi kuweka wazi nani na nani ataanza kesho (leo) hilo ni jambo ambalo wanapaswa kufahamu wachezaji wenyewe, tunahitaji ushindi kwa sababuSimba imepania kutwaa ubingwa msimu huu ili kuirejesha kwenye ushiriki wa mashindano ya kimataifa," alisema Omog raia wa Cameroon.

Omog leo anaweza akaanza na mfumo wa kutumia washambuliaji watatu mbele na viungo watatu (4-3-3) ambapo Ibrahim Ajib, Laudit Mavugo na Juma Luizio watapangwa kwa pamoja safu ya ushambuliaji.

Wakati Omog akijanasibu hivyo, Kocha wa Yanga, George Lwandamina, alisema mchezo wa leo utakuwa mgumu hasa kutokana na umuhimu wake.

"Hautakuwa mchezo rahisi, lakini tunafahamu tunapaswa kushinda ili kukoleza kasi yetu kuelekea kwenye ubingwa, wenzetu pia wamejiandaa kwa ajili ya mchezo huu na ndio maana nasema hautakuwa mchezo rahisi," alisema Lwandamina.

Kocha huyo Mzambia, alisema kitu cha msingi wachezaji wake wanafahamu umuhimu wa mchezo wa leo hivyo wataingia Uwanjani kupambana kwa ajili ya ushindi.

Kwa kufahamu ugumu wa mchezo wa leo, Lwandamina huwenda akaanza na mfumo wa kuweka viungo wanne katikati huku akiwaacha washambuliaji wawili mbele (4-4-2).

Polisi waimarisha Ulinzi

Wakati kumbukumbu za vurugu zilizotokea kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Oktoba Mosi mwaka jana zikiwa bado kwenye vichwa vya wadau wengi wa soka nchini, Jeshi la Polisi limetangaza 'vita' mashabiki watakaofanya fujo kwenye mchezo huo.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro amesemaJeshi hilo safari hii halitamfumbia macho mtu yeyote atakayefanya vitendo vya uharibifu au uvunjifu wa amani kama ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita.

Alisema vurugu zilizotokea kwenye mchezo wa kwanza sio tu ziliharibu uwanja pia zilidhalilisha Jeshi la Polisi.

"tumeweka askari wa kutosha kuanzia nje ya uwanja hadi maeneo wanakokaa mashabiki,” alisema.

Alisema hakuna shabiki atayeruhusiwa kuingia uwanjani na chupa yoyote ya maji kwa kuwa wengi wao wanatumia chupa hizo kuingia na vileo uwanjani.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments