Washambuliaji wa Yanga tishio Afrika

Unknown | 3:33 PM | 0 comments

Moroni. Washambuliaji wa Yanga, wametingia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwa ndiyo timu pekee iliyofunga mabao mengi katika mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mechi za mwishoni mwa wiki.

Yanga iliyokuwa Visiwa vya Comoro, iliichapa Ngaya Sports mabao 5-1 na kujiweka katika nafasi nzuri kucheza raundi ya kwanza, ikizisubiri APR ya Rwanda na Zanaco ya Zambia zilizotoka suluhu mchezo wa kwanza mjini Lusaka.

Mchezo huo wa Yanga ambao ulizalisha mabao sita, unafuatiwa na mchezo wa Al Ahly Tripoli (Libya) iliyoifunga Wa All Stars ya Ghana mabao 3-1 na mchezo wa Kadiogo (Burundi) iliyoifunga 3-0 Diables Noirs ya Congo sawa na Tanda (Ivory Coast) iliyoilaza ASFAN ya Nigeria mabao 3-0. Timu nyingine ambazo washambuliaji wake walifunga mabao mawili ni Cotonsport (Cameroon) iliyoifunga 2-0 Atlabara ya Sudan Kusini, Saint-Louisienne (Reu Union) iliifunga 2-1 Bidvest Wits (Afrika Kusini) huku CF Mounana (Gabon) ikiirarua Vital’O ya Burundi mabao 2-0.

Mechi nyingine, Zimamoto ya Zanzibar iliitungua Ferroviario Beira (Msumbiji) mabao 2-1, huku Cote d’Or ya Shelisheli ikiumbuka nyumbani kwa kuchapwa mabao 2-0 kabla ya CNaPS Sport ya Madagascar kuiadhibu Township Rollers ya Botswana kuilaza mabao 2-1.

Mchezo wa juzi, kiungo wa Yanga, Justine Zullu alifunga bao lake la kwanza tangu alipojiunga Yanga katika dakika 43 na dakika mbili baadaye Saimon Msuva alifunga bao la pili.

Mshambuliaji Obrey Chirwa alipachika bao la tatu dakika 59, kabla ya Mrundi Amiss Tambwe kufunga bao la nne. Thaban Kamusoko alihitimisha bao la tano katika dakika 73.

Bao la Ngaya lilipatikana dakika ya 66 likifungwa na Said Anfane Boura aliyetokea benchi.

Mipango mkakati ya Yanga

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema katika msimu huu wamejipangia jambo moja kubwa kwamba kupunguza ugumu katika mechi zao za Kimataifa lazima wafanye vizuri katika mechi ya kwanza bila kusubiri mchezo wa marudiano.

Mwambusi alisema akili yao hiyo inakuja kutokana na wingi wa mechi za karibu ambazo wanacheza sasa na hilo litapunguza ugumu katika mchezo wa marudiano ambao unaweza kuwachosha kabla ya mechi za ligi.

Alisema mpango huo hautajalisha Yanga inaanzia wapi na akili yao ni kuhakikisha hawatumii nguvu nyingi katika mechi za marudiano endapo watakuwa wamepata matokeo ya kuridhisha katika mechi ya kwanza.

“Unaona mechi zilivyo karibu sasa kuepuka ugumu ni lazima tufanye vizuri mechi za kwanza kama hii ili unapokuja mchezo wa marudiano tusitumie nguvu nyingi hili litatusaidia sana,” alisema Mwambusi. “Tuna majukumu mengi ratiba inaonyesha kwamba tunapocheza mchezo kama huu tutarudiana nao wiki inayofuatia na baada ya mechi ya hapo tunarudi katika ligi kawaida sasa ni lazima tuwe makini katika hilo tunataka kufanya makubwa ndiyo maana tunabadilisha mambo.

Kocha Ngaya atoa kauli

Kocha Mkuu wa Ngaya, Louis Mshangama amesema kupata kwake mikanda ya Yanga hakukuweza kuisaidia timu yake na kwamba uzoefu ndiyo umewafungisha.

Akizungumza na gazeti hili Mshangama alisema Yanga ilikuwa imara kutegua mitego yote ya timu yake na kwamba kila walipojipanga walizidi kujiweka katika wakati mgumu.

Alisema safu ya kiungo ya Yanga iliwapa wakati mgumu wachezaji wake na kujikuta wakipoteana na kwamba kikosi hicho cha wageni wao kilikuwa bora.

Mshangama alisema kwa sasa anataka kujipanga vyema kwa mchezo wa marudiano ambao amegundua makali kadhaa kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa Yanga na kwenda kuyafanyia kazi

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments