KAPOMBE MCHEZAJI BORA LIGI KUU
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
BEKI anayeweza kucheza nafasi za kiungo pia, Shomary Kapombe(pichani kulia) wa Azam FC ya Dar es Salaam ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mwezi Januari 2016.
Katika mwezi huo uliokuwa na raundi tatu, Kapombe alicheza dakika zote 180 za mechi mbili za timu yake dhidi ya African Sports na Mgambo Shooting. Mechi ya tatu ya Azam FC katika raundi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa kiporo, na ilichezwa Februari24, 2016.
Kapombe alifunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 wa timu yake dhidi ya Mgambo Shooting. Pia alisaidia kupatikana bao la Azam kwenye mechi dhidi ya African Sports iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, na mara nyingi mashambulizi ya timu yake yalianzia upande wake.
Washindani wa Kapombe kwenye kinyang'anyiro hicho katika mwezi huo walikuwa mshambuliaji wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Jeremiah Juma na beki wa Coastal Union ya Tanga, Miraji Adam.
Kwa kutwaa tuzo hiyo, Kapombe atazawadiwa kitita cha Sh. Milioni 1 na wadhamini wa Ligi hiyo, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Limited.
Category: tanzania
0 comments