RWANDA YAING’OA SUDAN KWA MATUTA NA KUTINGA FAINALI

Unknown | 7:46 PM | 0 comments


RWANDA imetinga fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kuifunga Sudan kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Ethiopia, dakika 90 zilimalizika kwa sare ya 0-0, ingawa Sudan ilicheza pungufu tangu dakika ya 21 baada ya Babkri Babeker kutolewa kwa kadi nyekundu.

Rwanda nayo ilimpoteza Isale Songa mwanzoni mwa dakika za nyongeza aliyetolewa kwa kadi nyekundu baada tu ya kuingia.


Sudan walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 100 kupitia kwa Atahir Babikir aliyemalizia pasi ya Mahir Idriss.

Amavubi ilisawazisha dakika ya 110 kupitia kwa kiungo wa Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza aliyemalizia pasi ya kichwa ya Jacques Tuyisenge kufuatia ‘majaro’ ya kiungo wa Yanga SC, Haruna Niyonzima.

Niyonzima akaenda kumfunga kipa hodari wa Sudan, Ekram Salim katika penalti ya kwanza na kuwatilia ‘baraka’ Ernest Sugira, Jacques Tuyisenge na Djihad Bizimana wakafunga pia.

Penalti za Sudan zilifungwa na Ibrahim Hassan na Mohammed Osman, wakati ya Atahir Babikir iliokolewa na kipa Olivier Kwizera na ya Mazin Ahmed ilitoka nje.

Amavubi iliyowang’oa mabingwa watetezi pia, Kenya katika Robo Fainali, sasa inasubiri mshindi kati ya Uganda na Ethiopia ikutane naye katika Fainali keshokutwa.
 
Credit: Bin Zubery

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments