YAW BERKO ASAINI MIEZI SITA SIMBA SC, DHAIRA NJE MSIMBAZI

Unknown | 11:51 PM | 0 comments

 


Na Prince Akbar, Mbezi
KIPA mkongwe wa Ghana, aliyewahi kudakia klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam, leo amesaini Mkataba wa miezi sita kuchezea wapinzani wa jadi, Simba SC.
Berko aliyetua leo Dar es Salaam akitokea Ghana nyumbani kwao, anachukua nafasi ya kipa Mganda, Abbel Dhaira ambaye anaachwa.
Berko aliidakia Yanga tangu mwaka 2010 baada ya kujiunga nayo katika dirisha dogo, Desemba mwaka 2009 akitokea Liberty Proffessionals ya Ghana hadi msimu uliopita alipotolewa kwa mkopo FC Lupopo ya DRC.
Berko kulia akisaini Mkataba mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe Mbezi, Dar es Salaam mchana wa leo

Hata hivyo, Berko alipofika Lubumbashi na kujionea hali halisi ya klabu hiyo, akakataa kuichezea na kurejea Yanga SC, ambao waliamua kuvunja naye Mkataba na kumlipa haki zake, hivyo akarejea Ghana.
Lakini kutokana na kumbukumbu ya kazi nzuri aliyoifanya Yanga SC, watani wa jadi wameona bora wamchukue- badala ya Dhaira, ambaye amekuwa akifungwa mabao rahisi.
Haswa Yanga iliamua kuachana na Berko baada ya kuridhishwa na uwezo wa kipa iliyemsajili kutoka Simba SC msimu uliopita, Ally Mustafa ‘Barthez’.
Hata hivyo, tayari Barthez naye amekwishaanza kuonekana ‘si mali kitu’ Jangwani na klabu hiyo imemsajili kipa mkongwe nchini, Juma Kaseja aliyeachwa Simba SC msimu huu.
Yanga sasa ina makipa watatu ambao wote wamewahi kudaka pamoja Simba SC, mbali na Barthez na Kaseja, yupo pia Deo Munishi ‘Dida’. 
Yaw Berko alizaliwa Oktoba 13, mwaka 1980 mjini Accra na alianzia soka yake Liberty Professionals FC kabla ya Januari mwaka 2005 kutolewa kwa mkopo klabu ya Pisico Binh Dịnh F.C. ya Vietnam, ambako baada ya mwaka mmoja alirejea Liberty kabla ya Desemba 2009 kuja Yanga SC.
Berko aliletwa nchini na kocha wa zamani wa Yanga, Mserbia, Kostadin Bozidar Papic ambaye alimuona mlinda mlango huyo wakati anafundisha Hearts Of Oak ya huko mwaka 2008.
 
Credit: Bin Zubeiry

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments