SIMBA NDIO JEMBE, YANGA YAGEUZWA MPINI
Wachezaji wa Timu ya Simba na baadhi ya viongozi wao wakipozi na kombe lao baada ya kukabidhiwa kwa kuifunga Timu ya Yanga Mabao 3-1 katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jioni ya leo.Mabao ya Simba yalifungwa na Hamis Tambwe mawili na Ramadhan Singano huku la kufutia machozi la Yanga likifungwa na Emmanuel Okwi.Picha zote na Othman Michuzi.
Meneja wa Yanga, Afidh Ally akipokea mfano wa hundi ya zaidi sh. 98 milioni Kwa kuibuka washindi katika shindano la Nani Mtani Jembe kwa kupata kura nyingi katika unywaji wa bia ya Kilimanjaro.
Hundi ya Simba ilisomeka hivi pamoja na Ushindi Mkubwa walioupata dhidi ya wapinzani wao.
Mgeni Rasmi katika Mchezo huo,Waziri wa Sheria na Katiba,Mh. Mathias Chikawe akikabidhi Kombe la Ushindi wa Nani Mtani Jembe kwa Nahodha wa Timu ya Simba mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa,Jijini Dar es Salaam.
Mshambuliaji wa Timu ya Yanga,Mrisho Ngassa (17),akiwa mpiga chenga ya Mwili Beki wa Timu ya Simba,Donald Mtosi wakati mchezo wao wa Nani Mtani Jembe unaoendelea hivi sasa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Hadi hivi sasa Simba wanaongoza kwa Bao 1-0 na tayari dakika 35 za mchezo zishakatika.Picha zote na Othman Michuzi.
Golikipa Machachari wa Timu ya Simba,Ivo Mapunda akiruka juu kudaka mpira uliokuwa unaelekea langini kwake.
Simba wakiandika Bao la Kwanza mnamo dakika ya 19 ya mchezo.
Mashabiki wa Simba.
Nahodha wa Timu ya Simba,Henry Joseph Shindika akikabiliana na Mpinzani wake wakati wa Mtanange wa Nani Mtani Jembe uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,jioni ya leo.
Kelvin Yondani wa Yanga akitoa pasi nzuri.
Sehemu ya mashabiki wa Yanga, waliokwisha keti katika siti zao wakisubiri kuishangilia timu yao.
Sehemu ya mashabiki wa Simba, waliokwisha keti katika siti zao wakisubiri kuishangilia timu yao.
********
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
SHUGHULI pevu ya mechi ya `NANI MTANI JEMBE?` baina ya wekundu wa Msimbazi Simba, `Taifa Kubwa` dhidi ya watani wao wa jadi, Dar Young Africans, imemalizika jioni hii kwa Mnyama kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1, kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.
Simba waliocheza mpira safi na kuwazidi maarifa Yanga walioongozwa na nyota wao wote wameandika mabao yao kupitia kwa kwa nyota wake Amis Tambwe aliyefunga mawili pamoja na kiungo Awadh Juma Issa.
Katika mchezo huo, Yanga ilimaliza pungufu baada ya beki wake, Kevin Yondan kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano, baada ya kumchezea rafu Ramadhani Singano ‘Messi’.
Bao la wana Jangwani limefungwa na mshambuliaji wao Mpya Emmanuel Anord Okwi aliyeingia kuitumikia klabu hiyo kwa mara ya kwanza tanga asajili desemba 15 mwa huu akitokea klabu ya SC Villa ya Kampala Uganda.
Leo hii kiukweli, Yanga waliingia kwa kujiamini zaidi kutokana na kikosi chao kusheheni nyota wengi wakiwemo, Okwi, Kiiza, Ngassa, Didier Kavumbagu, Niyonzima na wengine wengi wenye majina.
Hata hivyo Yanga kama kawaida yao walicheza soka la kujiamini na kuonesha kuwa wanajua zaidi kupiga mpira wa burudani `Show Game`.
Simba wao waliingia kwa kazi moja ya kutafuta ushindi ikizingatiwa wamekuwa wakichukuliwa kirahisi na watani zao wa jadi kufuatia kuwa na mabadiliko mengi kikosini.
Simba walionakena kuwa dhaifu kwa maneno ya watu na nje ya uwanja, lakini wamecheza soka safi zaidi ya Yanga na kufanikiwa kuwafunga mabao hayo.
Juma Kaseja kaanza vibaya na hii imeanza kuamsha maneno miongoni mwa mashabiki wa Yanga, lakini ni matokeo ya mpira, sema yamekuja wakati mbaya kwake.
Yawezekana baadhi ya mashabiki watawatupia lawama baadhi ya wachezaji wa Yanga, ila ni matokeo ya mpira na wamefanya makosa makubwa matatu na kufungwa.
Yanga kwa mara kadhaa walipata nafasi za kufunga, lakini kukosa umakini kumewagharimu.
Kwa upande wa mlinda mlango mpya wa Simba SC, Ivo Philip Mapunda ameonekana kuimarika zaidi na kuwa bora kwa wakati wote akiwa langoni.
Wakati watu wengi wakidai Ivo kazeeka, leo hii imedhihirisha kuwa utu uzima dawa, kwani ameokoa michomo mingi zaidi kutoka kwa washambuliaji wa Yanga.
Amis Tambwe alisema lazima awafunge Yanga, hatimaye kwa mara ya kwanza amefunga mabao mawili mawili muhimu katika ushindi mtamu kwa Mnyama.
Pia kocha mpya wa Simba SC, Mcroatia, Zdravko Logarusic ameiongoza Simba kwa mechi ya pili na kushinda zote.
Hivi karibuni aliiongoza klabu yake katika mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya KMKM Ya Zanzibar na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kikosi cha Yanga leo: Juma Kaseja, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza.
Wachezaji wa Akiba: Deo Munishi ‘Dida’, Oscar Joshua, Juma Abdul, Simon Msuva, Rajab Zahir, Hassan Dilunga, Emmanuel Okwi, Jerry Tegete, Relliant Lusajo, Nizar Khalfan, Hamisi Thabit na Said Bahanuzi.
Kikosi cha Simba SC; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Haroun Chanongo, Henry Joseph, Amisi Tambwe, Said Ndemla na Awadh Juma.
Wachezaji wa akiba: Yaw Berko, Omary Salum, William Lucian ‘Gallas’, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Ramadhani Singano ‘Messi’, Zahor Pazi na Amri Kiemba.
Wachezaji wa akiba: Yaw Berko, Omary Salum, William Lucian ‘Gallas’, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Ramadhani Singano ‘Messi’, Zahor Pazi na Amri Kiemba.
Category: tanzania
0 comments