RAGE AKUBALI KUJIUZULU
Kwa takriban mwezi sasa hali imekuwa si shwari ndani ya Simba, baada ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya Utendaji wakiongozwa na Kaimu makamu mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ kumsimamisha Rage kwa tuhuma mbalimbali.
Hata hivyo, Rage alikataa hatua hiyo na kusema kwamba yeye ni Mwenyekiti halali wa Simba, pamoja na hilo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimtaka Rage kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama ili kutatua tatizo hilo, lakini Rage aligoma na kusisitiza kuwa endapo TFF itamlazimisha kufanya hivyo atajiuzulu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rage ambaye hakuwepo nchini kwa takribani wiki tatu zilizopita, alisema hali ilivyo kwenye kamati ya utendaji hawawezi kufanya kazi pamoja hivyo ili kuinusuru Simba ni bora wajiuzulu wote kisha uchaguzi uitishwe mapema Januari na wanaoitakia mema klabu hiyo kugombea.
Rage alisema kwanza hana sababu ya kujiuzulu wala kuitisha mkutano wa dharura kwa sababu wanachama wanaompigia kelele ni wa tawi la Mpira pesa pekee.
“Haiwezekani katika matawi 78 tawi moja tu kila siku wanaongea, wangeongea matawi 78 kidogo ningeshtuka, mimi nimechaguliwa na watu 1,820 sasa tawi la Mpira pesa sijui lina watu 204 sijui 100 ila hata sielewi lina watu wangapi,haliwezi kunipa taabu,’… “Sina mpango wa kuitisha mkutano wa dharura kama hali itaendelea hivi ya kutoelewana njia nyepesi ninayoona mwanangu (akimaanisha mwandishi aliyezungumza naye) ni kuitisha mkutano wa uchaguzi Januari kabla ya tarehe 27, ili upatikane uongozi mpya kuanzia Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya utendaji”.
“Tusidanganyane bwana, kamati ya utendaji hatuwezi kufanya kazi pamoja kutokana na haya yaliyotokea, ninachokifanya ni kupitia vizuri katiba inasemaje kisha nitaandika barua ya kamati ya utendaji kujiuzulu, kisha tuitishe uchaguzi Januari,” alisema Rage.
Aidha Rage alisema, pia anasubiri uamuzi wa TFF kuhusu malalamiko yake maana aliandika barua kuomba kamati ipitie maamuzi yake ya mwanzo baada ya kuona kulikuwa na dosari, na kwamba kama wakirekebisha dosari alizoziona, atakuwa tayari kufuata maagizo yao.
“Mimi binafsi siwezi kufanya kazi na kamati ambayo tayari ilishanituhumu na kunisimamisha, kwa hiyo tayari hawana imani na mimi, sasa mimi imani na wao natoa wapi, kwa hiyo tutakuwa hatuwatendei haki wanachama wa Simba. Sasa ili tuonekane wote tunafuata maadili basi ni vyema kuanzia Mwenyekiti na Wajumbe wote wa kamati ya utendaji tukajiuzulu, tukaitisha mkutano wa uchaguzi ili kuiokoa klabu yetu ili ipate mafanikio makubwa”.
CHANZO NI HABARI LEO
Category: tanzania
0 comments