KOMBE LA MAPINDUZI: KOCHA WA ITALIA PRANDELLI MGENI RASMI SIMBA VS AFC LEOPARDS
Na Baraka Mpenja, Dar es
salaam
MAANDALIZI ya kombe la
Mapinduzi linalotarajia kuanza kutimua vumbi januari mosi mwakani yanakwenda
vizuri na timu zote zilizothibitisha kushiriki zinatarajia kuwasili desemba 31
mwaka huu.
Msemaji wa kamati ya
mashindano , Farouk Karim amesema kuwa timu za Tusker fc, AFC Leopard za Kenya,
KCC, URA za Uganda , Simba sc, Yanga, Azam fc na Mbeya City za Tanzania bara
tayari zimeshathibitisha kushiriki na kamati ya maandalizi imeshakamilisha
taratibu za kuzipokea.
SIMBA imepangwa kufungua pazia la michuano ya Kombe la
Mapinduzi kwa kucheza na AFC Leopards ya Kenya Januari Mosi wakati Yanga
wakishuka dimbani siku inayofuata kuikabili Tusker FC.
Karim amesema mgeni
rasmi katika mechi ya ufunguzi itakayopigwa januari mosi majira ya saa mbili
usiku katika uwanja wa Aman kisiwani Unguja baina ya Simba sc dhidi ya AFC
Leopard ya Kenya atakuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Italia, Cesare
Prandelli.
Pambano la Simba na Leopards litatanguliwa na mechi
kati ya wenyeji KMKM na KCC ya Uganda litakalopigwa saa 10 jioni kwenye uwanja
huohuo.
“Ninavyozungumza na wewe
muda huu, Prandelli yupo hapa Zanzibar mapumzikoni na tayari amekubali kufungua
michuano hii yenye maana kubwa katika miaka 50 ya mapinduzi ya Zanzibar”.
Alisema Karim.
Karim alisema katika
michuano ya mwaka huu viwanja viwili vitatumika ambavyo ni Gombani kisiwani
Pemba na Aman Kisiwani Unguja.
“Uwanja wa Gombani upo
katika hali nzuri na unavyojua una nyasi za bandia. Uwanja wa Aman umefanyiwa
ukarabati mkubwa na hivi sasa wataalamu kutoka China wapo hatua za mwisho kabisa
kukamilisha shughuli yao”. Alisema Karim.
Mratibu huyo alitoa wito
kwa wadau, wapenzi wa soka visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi kwani kamati
ya mashindano inategemea mapato ya milangoni kufanikisha
mipango.
“Michuano hii inagharimu
zaidi ya shilingi milioni 600, hatuna fedha hizo, tunategemea mapato ya
milangoni, hivyo mashabiki kufika kwao kwa wingi ndio mafanikio yetu”. Aliomba
Karim.
Aidha ameziomba taasisi
na makampuni ya bara na visiwani kujitokeza kufanya matangazo katika michuano
hiyo ili angalau wapate pesa za kuendeshea michuano
hiyo.
Michuano iliyopita, Azam
fc walitwaa ubingwa, lakini mwaka huu kuna changamoto mpya hasa kutokana na
uwepo wa timu za Dar Young Africans na Mbeya City ambazo
hazikushiriki.
Mechi zote za hatua ya makundi na robo fainali
zitafanyika kwenye viwanja wa Gombani Pemba na Aman Unguja, wakati nusu fainali
na fainali zitapigwa kwenye Uwanja wa Amani.
Katika michuano
iliyopita Simba waliishia nusu fainali baada ya kuondolewa na Azam FC kwa
mikwaju ya penalti 5-4 baada ya mechi kumalizika kwa sare ya 2-2 hata baada ya
kuongezwa dakika 30.
Category: tanzania
0 comments