AZAM FC YAIBAMIZA RUVU SHOOTING 3 - 0
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel; 0712461976 au 0764302956
Mechi
ya kujaribu matumizi ya tiketi za elektroniki kati ya Azam na Ruvu
Shooting iliyofanyika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam
jioni ya leo imemalizika kwa wana Lambalamba kuibuka na ushindi wa mabao
3-0 dhidi ya vijana wa Charles Boniface Mkwasa.
Azam
fc ikiwa chini ya kocha mpya, Mcameroon, Joseph Marius Omog iliandika
bao lake la kwanza katika dakika ya 10 kupitia kwa Mshambuliaji wake
hatari na nahodha, John Raphael Bocco kufuatia kazi nzuri ya Mganda,
Brian Umony .
Dakika
ya 30, mshambuliaji wa Azam fc, Raia wa Ivory Coast, Kipre Herman
Tchetche aliandika bao la pili kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya
Ayoub Kitala kuurudisha kwa mkono mpira uliokuwa unaelekea nyavuni. .
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Azam fc walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi
hicho cha kwanza, timu zote zilicheza soka la kufundishika, hivyo
kuleta burudani kubwa kwa mashabiki waliojitokeza kutazama mechi hiyo.
Kipindi
cha pili timu zote zilifanya mabadiliko kwa takribani vikosi vizima na
mshambuliaji mpya wa Azam kutoka Pwani ya Magharibi mwa Afrika, Ivory
Coast, Muamad Ismael Kone alikuwa kivutio baada ya kugusa nyasi za
Chamazi.
Kone
alionekana kucheza soka zuri na katika dakika ya 57 alifunga bao la tatu
na kukamilisha ushindi wa 3-0 leo hii kwa matajiri wa `Ice Cream`..
Refa
Israel Mujuni Nkongo alimpa kadi nyekundu beki wa Ruvu na kuifanya timu
ya Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ imalizie dakika 50 za pambano hilo
ikiwa pungufu.
Mechi
nyingine ya majaribio itakuwa kati ya Ashanti United na JKT Ruvu ambayo
itachezwa Januari Mosi mwakani kwenye uwanja huo huo.
Baada
ya Mchezo huo, kocha Omog alisema ana kazi kubwa ya kufanya kwani timu
inapoteza mipira kirahisi, haina kasi na inapopoteza mipira wachezaji
wanategeana kukaba.
Alisifia kikosi cha Azam FC kuwa
kina wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu na akasema hadi utakapofika
muda wa kucheza michezo ya kimtaifa anadhani timu itakuwa tayari.
Mchezo wa leo ulikuwa muhimu kwa kocha wa Azam fc kwani alikuwa
anakiangalia kikosi chake kinachojiandaa kushiriki mashindano ya kombe
la Mapinduzi inayotarajia kuanza januari mosi mwakani.
Mbali
na Azam fc, klabu ya Yanga, Simba na Mbeya City zilithibitisha
kushiriki michuano hiyo muhimu kwa timu hizo kuandaa vikosi vyao
kuelekea ngwe ya pili ya ligi kuu soka Tanzania bara inayotarajia kuanza
kushika kasi januari 25 mwakani.
Yanga wao wana kazi kubwa kwani februari mwakani wanaingia katika kibarua cha ligi ya mabingwa barani Afrika.
Wao
Ruvu Shooting chini ya kocha mkuu, Charles Boniface Mkwasa `Masta`
wanarejea zao kambini kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania
bara.
Category: tanzania
0 comments