Mechi ya Simba na Azam ipo pale pale ... Uwanja ndio umebadilishwa
Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kati ya Azam FC na Simba ya Dar es Salaam, utafanyika Jumamosi Septemba 17, 2016 kama ilivyopangwa awali.
Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam badala ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa sababu za kuipa nafasi timu ya taifa ya vijana ya mpira wa miguu ya Congo Brazzaville ambayo itakuwa nchini kwa ajili ya mchezo wa ushindani dhidi ya wenyeji – Serengeti Boys ambayo ni timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
Timu hizo zinakutana kwenye mchezo wa kwanza wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo. Mchezo huo utafanyika Septemba 18, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam hivyo kutokana na kanuni za mashindano, siku moja kabla mgeni anapata nafasi ya kufanya mazoezi.
Serengeti Boys ambayo ilipiga kambi Shelisheli kujiandaa na mchezo huo ambako imejipanga vyema kuiondoa Congo Brazzaville katika michezo miwili inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali ukianzia huo wa Septemba 18, 2016 kabla ya kurudiana jijini Brazzaville hapo Septemba 30 au Oktoba 1 au Oktoba 2, mwaka huu.
Mtendaji Mkuu wa (CEO) Azam FC, Saad Kawemba kwa mujibu wa kanuni ya 6 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kipengele cha 5 na 6, ameridhia mchezo huo kufanyika Uwanja wa Uhuru hapo Septemba 17, 2016 na kufuta upotoshwaji unaofanyika kwenye mitandao ya kijamiii.
Kawemba alizungumza hayo, mara baada ya kupokea Ngao ya Hisani halisi mara baada ya tuzo hiyo kufika jijini Dar es Salaam ikitokea China pamoja na vifaa vingine. Itakumbukwa kwamba awali Agosti 17, 2016 mara baada ya kuishinda Young Africans kwa mikwaju ya penalti, Azam walipewa Ngao ya mfano.
Category: tanzania
0 comments