YANGA YA KIMATAIFA USHINDI KAMA KAWA ... YAIPIGA VIWILI APR

Unknown | 11:23 PM | 0 comments

Na Prince Akbar, KIGALI
YANGA SC imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuingia hatua ya mwisho ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji APR katika mchezo wa kwanza wa raundi ya Kwanza jioni ya leo Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda.
Asante kwa wafungaji wa mabao hayo, beki Juma Abdul Jaffar kipindi cha kwanza na kiungo Thabani Scara Kamusoko kipindi cha pili na Yanga sasa watahitaji hata sare mchezo wa marudiano ili kusonga mbele.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Duncan Lengani, aliyesaidiwa na washika vibendera Clemence Kanduku na Jonizio Luwizi wote wa Malawi, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.


Bao hilo lilifungwa na beki wa kulia aliye katika kiwango kizuri kwa sasa, Juma Abdul Jaffar dakika ya 20 kwa shuti la mpira wa adhabu ndogo umbali wa mita 30, baada ya Nahodha wa leo wa Yanga, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kuangushwa.
Yanga iliyokuja na mashabiki wapatao 100 kutoka Dar es Salaam walioongezewa nguvu na mamia ya mashabiki wa mahasimu wa APR, Rayon walitawala mchezo kipindi cha kwanza na ilikuwa vigumu kuamini kama APR walikuwa nyumbani.
Kipindi cha pili, kidogo APR walikianza vizuri na kuonekana kama wangeweza kusawazisha, lakini bado nyota ya Wana Jangwani iliendelea kung’ara Kigali.
Kiungo Thabani Scara Kamusoko akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 74 akimalizia pasi ya Mzimbabwe mwenzake, mshambuliaji Donald Dombo Ngoma.
Baada ya bao hilo, Yanga wakajiamini zaidi na kujikuta wanaizawadia bao rahisi APR dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida lililofungwa na Patrick Sibomana. 
Mchezo wa marudiano utafanyika wiki moja baadaye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na utachezeshwa na marefa wa Shelisheli; katikati Bernard Camille na pemebeni watakuwapo Eldrick Adelaide na Gerard Pool. 
Kikosi cha Yanga SC kilikwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji Mngwali, Pato Ngonyani, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Simon Msuva dk46, Donald Ngoma/Matheo Anthony dk88 na Haruna Niyonzima/Mbuyu Twite dk87.
APR; Oliver Kwizera, Rusheshangoga/dk88, Michael Rutanga, Eric Rwatubyaye, Abdul Emily, Bayisenge Yannick, Mukunzi Fiston/Mugenzi dk75, Nkinzingabo, Jihadi Bizimana/Benadeta dk77, Mubumbyi Bernabe, Iranzi Jean Claude na Patrick Sibomana. 

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments