TAARIFA ZA KIMICHEZO KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

Unknown | 10:17 PM | 0 comments


tff_LOGO1

SIMBA YAIKARIBISHA OLJORO JKT DAR
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania inaingia raundi ya 16 wikiendi hii kwa mechi nne ambapo kesho (Februari1 mwaka huu) Simba itakuwa mwenyeji wa Oljoro JKT katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ni sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A. Refa atakuwa Nathan Lazaro kutoka mkoani Kilimanjaro wakati Kamishna ni Hakim Byemba wa Dodoma.
Uwanja wa Azam uliopo Mbagala siku hiyo kutakuwa na mechi kati ya wenyeji Ashanti United na Mgambo Shooting kutoka Handeni mkoani Tanga kwa viingilio vya sh. 3,000 kwa sh. 10,000.
Jumapili (Februari 2 mwaka huu) ni Yanga vs Mbeya City (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, saa 10 kamili jioni), na Azam vs Kagera Sugar (Uwanja wa Azam Complex, Chamazi saa 10 kamili jioni).
Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Februari 5 mwaka huu) kwa mechi kati ya Tanzania Prisons vs Coastal Union (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Mgambo Shooting vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers vs Oljoro JKT (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), na JKT Ruvu vs Ashanti United (Uwanja wa Azam Complex, Chamazi).

SERENGETI BOYS YAPANGIWA AFRIKA KUSINI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) itacheza na Afrika Kusini katika mechi za mchujo kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Niger.
Serengeti Boys ambayo pamoja na nchi nyingine 17 zimeingia moja kwa moja katika raundi ya pili itaanzia mechi hiyo nyumbani kati ya Julai 18-20 mwaka huu wakati ile ya marudiano itafanyika nchini Afrika Kusini kati ya Agosti 1-3 mwaka huu.
Ikifanikiwa kuitoa Afrika Kusini, Serengeti Boys itacheza mechi ya raundi ya tatu na ya mwisho na mshindi wa mechi kati ya Misri/Sudan vs Congo Brazzaville.
Nchi nyingine ambazo zimeingia moja kwa moja raundi ya pili ni Afrika Kusini, Angola, Benin, Botswana, Burkina Faso, Congo Brazzaville, Ethiopia, Gabon, Ghana, Ivory Coast, Mali, Morocco, Nigeria, Rwanda, Senegal, Tunisia na Zambia.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kutangaza benchi la ufundi litakaloiongoza Serengeti Boys hivi karibuni.
TFF MPYA YATIMIZA SIKU 100
Kamati mpya ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Rais Jamal Malinzi, Februari 4 mwaka huu inatimiza siku 100 tangu iingie madarakani katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28 mwaka jana.
Hivyo, Rais Malinzi atazungumza na waandishi wa habari Februari 7 mwaka huu kuelezea utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi. Muda na mahali utakapofanyika mkutano huo mtaarifiwa baadaye.
BODI YA LIGI YAZIPIGA JEKI KLABU ZA FDL
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa sh. milioni 1.5 kwa kila klabu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Uamuzi wa kuzisaidia timu hizo ulifanywa katika kikao cha TPLB kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo fedha hizo zitalipwa kupitia kwenye akaunti za klabu husika. Hivyo klabu ambazo hazijawasilisha akaunti zao TPLB zinatakiwa kuwasilisha haraka.
Klabu za FDL ni African Lyon, Burkina Moro, Friends Rangers, Green Warriors, Kanembwa JKT, Kimondo, Kurugenzi Mafinga, Lipuli, Majimaji, Mkamba Rangers, Mlale JKT na Mwadui.
Nyingine ni Ndanda, Pamba, Polisi Dar es Salaam, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Morogoro, Polisi Tabora, Stand United, Tessema, Toto Africans, Trans Camp na Villa Squad.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments