MBEYA CITY FC WATEMA MKWARA MZITO
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel: o712461976 au 0764302956
WAKALI
wapya wa ligi kuu soka Tanzania bara, `The City Zambarao` au `nyuki wa
nyanda za juu kusini`,Klabu ya Mbeya City wapo chimbo maeneo ya
Mwakareli Tukuyu jijini Mbeya kujiandaa na ngwe ya lala kwa buriani ya
ligi kuu.
Kocha
msaidizi wa klabu hiyo, Maka Mwalwisyi amesema kuwa wanatarajia
kuongeza kasi zaidi ya ile ya mzunguko wa kwanza na ndio maana waliingia
kambini mapema kujiimarisha.
“Falsafa
yetu imejikita zaidi kutumia vijana, tulikaa na wachezaji wetu na
kuwaeleza umuhimu wa kubakia klabuni kutokana na mipango mizuri ya
kuwafikisha mbali zaidi. Hutujauza mchezaji hata mmoja, wote wapo
kambini na wanaendelea kujifua zaidi”. Alisema Maka.
Maka
alisema kuna timu kubwa zilishatupia ndoana wakati wa dirisha dogo la
usajili zikitaka kuwanasa vijana wetu, lakini tayari benchi la ufundi
lilishawatahadharisha wachezaji kuwa wanaweza kukimbilia fedha na
kujiunga na klabu kubwa na wakaishia kukalia benchi kama wenzao
waliotangulia.
Oyaaa
fanyeni hivi, sawa?: Kocha mkuu wa Mbeya City FC, Juma Mwambusi
(katikati) akiongea na vijana wake, Hassan Mwasapili (kushoto) na Peter
Richard (kulia) kwenye moja ya mazoezi yake mzunguko wa kwanza wa ligi
kuu soka Tanzania bara. Picha na Maktaba
“Yuko
wapi Said Bahanuz?, yuko wapi Hussein Javu aliyekuwa akitamba na
Mtibwa?. Walijiunga na Yanga, mambo yamekuwa magumu kwao, hawapati
nafasi. Tumewaeleza vijana wetu kuhusu mazingira hayo na wanaelewa”.
Alisema Maka.
Kocha
huyo aliongeza kuwa wanahitaji kuona vijana wao wanafikiria soka la
kulipwa ili wapate mafanikio makubwa kama ilivyo kwa Mbwana Ally Samatta
na Thomas Emmanuel Ulimwengu wanaocheza TP Mazembe ya Kongo na kuvuna
dola za kutosha.
Aidha
Maka alisema watu wengi waliwatabiria kuwa nguvu ya soda, lakini mpaka
ngwe ya mwisho ya mzunguko wa kwanza, tayari watu walishaanza kuwaogopa
na kuona wana dhamira ya kweli.
“Sasa
wanatusikilizia mzunguko wa pili. Sisi tuna wachezaji wengi wa kiwango
cha juu, na ndio maana leo hii unaweza kumuona Paul Nonga akicheza,
kesho ukamuona Jeremiah John au Mwagane Yeya akicheza nafasi ileile kwa
kiwango cha juu. Sasa tunakuja na kasi kubwa na sura mpya yaani
tutaongeza mara mbili zaidi”. Alisema Maka.
Mbeya
City ilikuwa timu tishio katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu na
kujizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa mashabiki ambao waliwafananisha
na Tukuyu Stars `Banyambala` ambao enzi zao walipanda ligi kuu na kutwaa
taji.
Klabu
hiyo inayonolewa na kocha mkuu Juma Mwambusi ilimaliza mzunguko wa
kwanza ikiwa na pointi 27 katika nafasi ya tatu sawa na Azam fc waliopo
nafasi ya pili wakiwa na pointi 27, huku Bingwa mtetezi Yanga akiwa
kileleni na pointi 28.
Nafasi
ya nne inakaliwa na watani wa jadi wa Yanga, wekundu wa Msimbazi Simba
ambao wameongeza sura mpya kikosini mwao wakiwemo Awadh Issa Juma kutoka
Mtibwa, Ivo Mapunda na Donald Mosoti Omwanwa kutoka Gor Mahia ya
Kenya, Pia yupo Kipa Yaw Berko raia wa Ghana na wengine.
Pia
wamebadili benchi la ufundi ambapo aliyekuwa kocha mkuu Alhaj Abdallah
Kibaden `King Mputa` na msaidizi wake Jamhuri Kiwhelo `Julio`
walifungashiwa virago na nafasi yao kuchukuliwa na kocha raia wa
Croatia, Zdravko Logarusic akisaidiwa na kiungo wa zamani wa klabu
hiyo, Seleman Abdallah Matola `Veron`.
Category: tanzania
0 comments