JULIO: KUFUKUZWA SIMBA NA KING WANGU KUMENIFANYA NIUCHUKIE MPIRA…LAKINI AZAM FC NAWATAMANI SANA!!

Unknown | 10:06 PM | 0 comments

 


JULIO
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel: 0712461976 au  0764302956
BAADA ya kufukuzwa kazi na klabu ya Simba SC, aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Jamhuri Kiwhelo `Julio` amesema kitendo hicho kimemfanya auchukiae mpira wa Tanzania kwa sasa.
Julio alisema wapo watu wanasababisha mambo haya kutokea. Si Rage hata kidogo bali kuna watu wanafanya umafia huu.
“Mimi simtetei Rage, hata haya mambo ya Okwi wapo wanaosababisha na si mwenyekiti. Mimi na King Kibadeni tumefukuzwa bila sababu. Hawakuwa na sababu yoyote ile. Njia anazoenda nazo Rage zinaweza kuleta tija kwa soka la klabu, tofauti na mawazo ya watu”. Alisema Julio.
Julio aliendelea kueleza kuwa huwezi kumfukuza kocha kwasababu timu iko nafasi ya nne katika msimamo wa ligi baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika.
“Ingekuwa kocha anafukuzwa kwasababu hiyo, angefukuzwa David Moyes ambaye timu yake ni ya tisa. Man United kuna watu wenye akili na pesa, lakini hawana mpango wa kumfukuza”. Alisema Julio.
Kocha huyo mwenye historian na  Simba alisisitiza kuwa mpira wa Tanzania unaendeshwa kinafiki na fitina, hivyo kufika mbali ni kuota mchana kweupe.
Aidha Julio alikiri kuwa kwa sasa Azam fc ndio klabu bora kuanzia mfumo wa uendeshaji  wa klabu pamoja na soka la vijana.
“Mimi Julio naipenda Simba sc, lakini ukiniuliza ni timu gani napenda kufundisha, nitakwambia ni Azam fc. Wanajali, wana misingi bora ya Uongozi na wana mipango mizuri sana ya soka la vijana, wanalipa fedha nzuri na ndio maana wanafanikiwa kuliko timu za Simba na Yanga zenye fitina nyingi”. Aliongeza Julio.
Pia kocha huyo alisisitiza kuwa timu za Simba na Yanga si mikono salama kwa makocha na wachezaji wa Tanzania kwasababu hazina mfumo maalumu wa kuendeleza soka la vijana na huwa zina maamuzi ya haraka kufukuza makocha.
“Wachezaji wetu wanakimbilia timu hizo kwa madai ya kutaka kufahamika na kupata fedha nyingi. Watafika pale, lakini hawatafika  wanapohitaji kwani kuna mambo ya ajabu katika klabu hizi. Si mikono salama hata kidogo”. Alisema Julio.
Julio aliunga mkono Jitihada za rais wa TFF, Jamal Malinzi kutaka timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars icheze fainali za mataifa ya Afrika 2015, lakini akakiri ugumu kwasababu hakuna mfumo mzuri.
“Hatuna shule za soka, mfumo mbaya wa uendesheji wa soka la vijana, mfano michuano ya copa coca cola, Uhai Cup inakuja kwa muda mfupi. Kwa msingi huu hatuwezi kufika sehemu yote”. Alisema Julio.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments