Kudadaki!:
Hawa wote wameshindwa kuwafurahisha Watanzania leo uwanja wa Taifa
dhidi ya Timu ya Taifa ya Zimbabwe na kulazimishwa suluhu, labda
wasubiri CECAFA
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
TIMU
ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha raia wa
Denmark, Kim Poulsen, leo imelazimishwa suluhu dhidi ya Zimbabwe katika
mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopo katika kalenda ya FIFA, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Stars
ulianza mchezo huo kwa uzuri kabisa huku safu ya kiungo iliyokuwa
ikiongozwa na nyota chipukizi, Hassan Dilunga, Frank Domayo na mzee wa
kazi, mtaalamu wa mashuti na kupiga pasi za ukweli, Mwinyi kazimoto
Mwitula ikifanya kazi yake vizuri.
Hata
hivyo dakika ya tisini ilikuwa chungu kwa mashabiki wa Taifa Stars
baada ya Zimbabwe kupachika bao safi kimiani kupitia kwa Sithole Simba,
lakini bahati nzuri mwamuzi wa kati Ronnie Kalema na wasaidizi wake
Samuel Kayondo na Lee Okelo wote raia wa Uganda kukataa bao hilo.
Mashabiki
wengi waliingia uwanjani wakiwa na matumaini ya kuona soka safi kwa
kikosi kilichokuwa na majembe yote ya kazi akiwemo Mbwana Ally Samata,
Thomas Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe
ya DRC, Mwinyi kazimoto anayecheza klabu ya Al Markhiya ya Qatar na
Shomari Kapombe anayechezea AS Cannes ya nchini Ufaransa, lakini mambo
yalikuwa magumu na wengi kunyimwa uhondo wa kupiga kidedea.
Dakika
za mwanzo Safu ya kiungo ya Stars ilifanya kazi nzuri sana kuwalisha
mipira washambuliaji wa Stars, Samata, Ulimwengu na Ngassa, ambao
walipata nafasi za kufunga, lakini wakashindwa kuzibadili kuwa magoli.
Dakika
10 baadaye Wazimbabwe walizinduka na kucheza soka la uhakika,
wakatengeneza nafasi za kufunga, lakini ugonjwa wao ulifanana na wa
Stars.
Cha
kufurahisha leo, ni uwezo wa kipa mkongwe aliyekuwa chaguo la kwanza la
Marcio Maximo, Ivo Mapunda kwani alionesha uhai na kuoko bunduki tatu
ambazo zingebadili hadithi.
Hata
hivyo tofauti na mechi za nyuma ambapo kocha mkuu wa Stars, Kim Poulsen
alikuwa anashangilia, leo hii mashabiki walionesha kukasirika na
kuzomea, huku wakisikika wakisema kocha huyo timu imemshinda hivyo
afungashe virago.
Wachezaji
wengi wanaounda Taifa Stars pia wamo katika kikosi cha Kilimanjaro
Stars (Timu ya Taifa ya Tanzania bara), hivyo wanaendelea na mazoezi ya
kujiandaa na michuano ya CECAFA inayoanza kutimua vumbi novemba 27 mwaka
huu, Nairobi Kenya.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa;; Ivo Mapunda, Shomari Kapombe, Erasto
Nyoni/Himid Mao dk56, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Frank Domayo, Hassan
Dilunga/Salum Abubakar dk51, Mwinyi Kazimoto/Amri Kiemba dk51, Thomas
Ulimwengu, Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa/Farid Mussa dk80.
Zimbabwe:
Tapiwa Kapini, Ocean Mushere, Carrington Nyandemba, Obey
Mureneheri/Misheck Mborai dk46, Themba Ndhlovu/Felix Chidungwe, Isaac
Majari/Patson Jaure, Kapinda Wonder, Kundawashe Mahachi, Warren
Dube/Nkosana Siwela, Lot Chiungwa/Gerald Ndhlovu na Simba Sithole
0 comments