RAGE, JULIO NA KIBADENI "OUT" SIMBA

Unknown | 6:21 AM | 0 comments

 


Ismail Aden Rage(1)
Je, kikao cha Harusi kitatajwa tena!?: Mwenyekiti wa Simba Sc, Alhaji Ismail Rage amesimamishwa, kinachosubiriwa sasa ni cheche zake
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam 
 Haya mambo mpaka lini?, haya sasa tuwaachie wafanye yao. 
Hakika Mgogoro mkubwa uko njiani katika klabu ya Simba sc baada ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji kukutana jana usiku na kuchukua maamuzi magumu ambayo yameanikwa leo kwa waandishi wa habari ofisi za shirikisho la soka Tanzania TFF, maeneo ya Karume, jijini Dar es salaam. 
Kikao hicho kilichofanyika bila ya uwepo wa mwenyekiti wa klabu hiyo ambaye ni mbunge wa jimbo la Tabora Mjini, Alhaji Ismail Aden Rage, kimeamua mazito yenye kila dalili ya kutibua na kukoroga mambo Msimbazi. 
Maamuzi hayo yaliyotangazwa leo na kaimu mwenyekiti wa klabu hiyo Joseph Itang`are `Mzee Kinesi` ni;
Kwanza kumsimamisha mwenyekiti wa klabu hiyo aliyechaguliwa kihalali na wanachama, Aden Rage kwa madai ya kukosa imani naye.
Hata hivyo mzee Kinessi ambaye amejikaimisha nafasi ya mwenyekiti kuanzia jana baada ya kikao hicho alishindwa kuweka wazi sababu za msingi za kumsimamisha Rage zaidi ya kueleza kuwa wamekosa imani naye.
Pili; kikao hicho kimefikia maamuzi ya kusimamisha benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu Alhaji Abdallah Athuman Seif `King Kibadeni Mputa` akisaidiwa na Jamhuri Musa Kiwhelu `Julio` kwa madai ya kutoridhishwi na uwezo wao.
Ndani ya mzunguko mmoja tu ambao Simba wamekuwa katika kipindi cha kutengeneza timu yao, tayari wameshamsimamisha kibadeni ambaye ni kocha pekee mwenye rekodi ya kuifisha klabu hiyo fainali za kombe la washindi barani Afrika, je, imetosha kufikia maamuzi hayo?.
Lakini mzee Kinessi alipoulizwa kuwa kikao hicho kimefanya mapinduzi?, alidai kuwa hapana, bali kimefanya hivyo kumsimamisha Rage kwa muda kusubiri mkutano mkuu ambao utaamua kumrejesha au kumuondoa.
Kuhusu kumsimamisha kibadeni, Kinessi alisema sio simba tu waliofanya mamauzi ya kuwatoa makocha wao, amewataja Azam fc, Coastal, Ashanti na akasisitiza kuwa hawawezi kumshikilia kocha anayeifanya timu iwe nafasi ya nne wakati ilianza ligi kwa kuongoza.
Kikao hicho kimemuudhinisha kocha wa Simba B, Suleiman Matola `Veron` kuwa kocha msaidizi mpaka kocha mpya atakapotangazwa desemba mosi. Matola ataanza kuiandaa timu kwa ajili ya mzunguko wa pili na michuano ya Mapinduzi mwakani.
Wasiwasi wangu ni kama maamuzi hayo yamefuata vigezo, kwani Rage aliaminiwa na wanachama waliomchagua kuwa mwenyekiti wao kwa kura nyingi, lakini watu wachache wanasema hawana imani naye. Yetu macho!.
Kinesi ambaye alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba na baadaye akachaguliwa kuwa kaimu mwenyekiti wa Simba baada ya aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Geofrey Nyange Kaburu kujiuzulu, iwaje leo atangaze kukaimu nafasi ya mwenyekiti?.
Kali zaidi maamuzi hayo yamefikiwa wakati mwenyekiti Rage hayupo nchini kwa sasa.
Ikumbukwe kuwa mapema mwaka huu baadhi ya wanachama walitangaza kumpindua Rage wakati huo akiwa India kupata matibabu, lakini baada ya kurejea wanachama wengi walijitokeza kumpokea uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere kishujaa na wakisema yeye ndiye mwenyekiti wao.
Lakini akiwa India, Rage alijibu mapigo ya wanachama wao kwa kudai kikao chao kilikuwa cha Harusi, sasa tusubiri na hili la leo ataongea nini.
Matatizo haya ya uongozi yamekuwepo kwa muda mrefu tangu Rage aingie madarakani, na kama yataendekezwa, basi timu itaendelea kuboronga.
Kikao kilifanyika jana Jumatatu, wakati Jumapili Rage alifanya zoezi la kusajili wachezaji wawili wapya, kiungo Awadh Juma na mshambuliaji Ally Badru, wote kutoka Zanzibar.
Kwanini Kinesi asingevuta subira mwenyekiti arejee ndio wafanye kikao?. Halafu amesema wameshatuma barau pepe kwa Rage na taarifa imetumwa TFF pia, tusubiri cheche za mpiganaji Rage.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments