Simba uso kwa uso na Yanga

Unknown | 10:19 AM | 0 comments


Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara watani zao mabingwa wa Kombe la FA, Simba watakutana katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ni maalum kwa ajili ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2017/18, ambao unatarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu kwenye viwanja saba hapa nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema pia timu hizo zitakutana katika mechi ya kwanza msimu ujao ifikapo Oktoba 14, mwaka huu ambayo Simba itakuwa mwenyeji na itakuwa ikishuka uwanjani na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 iliyoupata mechi ya mwisho zilipokutana.

Lucas alisema katika mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo, Simba itaanza kuwania ubingwa huo unaoshikiliwa na watani zao kwa kuwakaribisha Ruvu Shooting ya Pwani wakati Azam FC itaanzia ugenini kwenye Uwanja wa Nangwanda Mtwara kwa kuwavaa Ndanda FC wakati Mwadui FC itachuana na Singida United ambayo imepanda daraja msimu huu.

Alisema siku hiyo ya ufunguzi pia Mtibwa Sugar watawakaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Manungu huku Kagera Sugar ikikutana na majirani zao Mbao FC mjini Bukoba, Njombe Mji wakiwasubiri Tanzania Prisons huku Majimaji ya Songea wakiwafuata Mbeya City jijini Mbeya.

Mabingwa watetezi, Yanga wenyewe wataanza kutetea ubingwa wao Agosti 27, mwaka huu kwa kuwakaribisha Lipuli FC ya Iringa ambayo sasa iko chini ya nahodha na kiungo wa zamani wa Simba, Selemani Matola.

“Maandalizi ya ligi hiyo yako katika hatua nzuri, lakini tunazikumbusha klabu kuwa hatutaruhusu makocha ambao hawana sifa kuendelea kuziongoza timu hizo kwa mujibu wa kanuni ya 11 ambayo inataka kocha wa timu ya Ligi Kuu kuwa na leseni ya kuanzia Daraja B huku [wanaozinoa] Daraja la Kwanza ikiwa ni kuanzia Daraja C,” alisema Lucas.

Aliongeza kuwa kabla ya kuanza kwa ligi hiyo kutakuwa na semina na mitihani ya majaribio kwa waamuzi na msimu huu mchakato huo utafanyika katika kituo kimoja cha Dar es Salaam kuanzia Julai 28 mpaka 31, mwaka huu.

Aidha, aliwakumbusha viongozi wa timu zote 16 zinazotarajiwa kushiriki ligi hiyo kukamilisha taratibu za usajili wa wachezaji ambao dirisha lake litafungwa rasmi ifikapo Agosti 6, mwaka huu.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments