TFF yaipokonya point Simba
Hatimaye Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeipokonya pointi tatu Simba SC, ilizokuwa imepewa kutoka kwa Klabu ya Kagera Sugar.
Awali, Simba ilikuwa imepewa ushindi wa mezani wa pointi tatu na magoli matatu dhidi ya Kagera Sugar, baada ya mchezo wake na timu hiyo ya mkoani Kagera kumalizika ikiwa imepigwa magoli 2-1.
Ushindi huo wa mezani ulitokana na malalamiko kuwa Kagera Sugar ilimchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano, hivyo hakuwa na sifa za kushiriki mchezo huo kwa mujibu wa kanuni na sheria za Soka.
Akitangaza uamuzi wa kurejesha matokeo ya awali ya uwanjani leo katika ukumbi wa Habari wa TFF, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Selestin Mwesigwa alisema kuwa sababu zilizopelekea Kamati kuchukua uamuzi huo, ni pamoja na kucheleweshwa kwa malalamiko ya Simba SC dhidi ya Kagera Sugar, Simba kushindwa kulipia ada ya rufaa dhidi ya maamuzi ya mechi hiyo na kukosekana kwa uhalali wa Kamati ya Saa 72 kwa kuwahusisha wajumbe waalikwa ambao hawakuwa na sifa za kuwa kwenye kamati hiyo.
Kutokana na uamuzi huo, Simba imeendelea kuwa kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), ikiwa na pointi 59 badala ya 62 za awali.
Hali hiyo inawapa nafuu ya kupumua watani wao wa jadi, Young Africans ambao wana pointi 56 huku wakiwa na michezo miwili nyuma ya Simba FC.
Category: tanzania
0 comments