Samattah aanza kugombewa Ulaya
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta yuko mbioni kurithi mikoba ya mshambuliaji wa zamani wa Arsenal na Manchester United, Robin van Persie katika klabu ya Fenerbahce ya Uturuki.
Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji ni miongoni mwa wachezaji wanne wanaotafutwa na Fenerbahce katika dirisha lijalo la usajili, wengine ni Theo Bongonda, Ridgeciano Haps na Thomas Bruns
Uamuzi wa Fenerbahce kumtaja Samatta katika orodha yao ya usajili inaonekana kushangaza wengi barani Ulaya.
Hata hivyo, rekodi za Mtanzania huyo mwenye mkataba na Genk hadi 2020, katika msimu huu amefunga mabao 19 akitoa pasi tano za mabao katika mechi 49 alizocheza za mashindano yote hadi sasa.
Pia, hivi karibuni Samatta aliweka rekodi ya kufunga mabao matano katika mechi sita mfululizo rekodi inayoonyesha kuivutia zaidi Fenerbahce inayotaka kutengeneza kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Uturuki na mashindano ya Ulaya.
Kwa mujibu mtandao wa fotospor, Meneja Utawala wa Fenerbahce, Hassan Cetinkaya alikuwepo uwanjani kwenye mchezo wa kwanza wa Europa Ligi kati ya Celta Vigo na Genk kwa ajili ya kumtazama Samatta pamoja na mchezaji wa Celta Vigo, Theo Bongonda.
Kuingia kwa Samatta katika rada za Fenerbahce ni wazi siku za mkongwe Van Persie aliyebakiza miaka miwili zimeanza kuhesabika hasa baada ya kupungua kwa kasi yake ya kuzifumania nyavu msimu huu. Van Persie amefunga mabao sita katika mechi 25 alizoichezea Fenerbahce katika mashindano mbalimbali msimu huu.
Mbali ya Waturuki hao Samatta tayari ameanza kuzivutia timu za Ligi Kuu England pamoja na Ujerumani zinadaiwa kuwania saini yake mwisho wa msimu huu.
Klabu tatu za Ujerumani zinazoshiriki Bundesliga ni Wolsfburg, Hamburger SV na Borussia Moenchengladbach zimeonyesha nia ya wazi ya kutaka huduma ya Samatta.
Iwapo Samatta atafanikiwa kujiunga na Fenerbahce atakuwa pamoja na nyota kama Gregory Van Der Wiel, Raul Meirelles, Miroslav Stoch, Martin Skrtel, Emannuel Emenike, Simon Kjaer, Moussa Sow na Mehmet Topal huku wakifundishwa na kocha Dick Advocaat kutoka Uholanzi.
Category: uingereza
0 comments