Kichuya aipoka tonge Yanga
Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga wameshindwa kutamba baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Amissi Tambwe alifungia Yanga bao kuongoza katika dakika 26 baada ya kupokea kwa kifua pasi ndefu ya Mbuyu Twite na kumchambua kipa wa Simba, Vincent Angban, kuingia kwa bao hilo kulianzisha vurugu kutoka kwa mashabiki wa Simba walioamua kurusha viti uwanjani.
Furaha ya mashabiki wa Yanga ilipotea dakika 87, wakati chipukizi Shiza Kichuya alipoifungia Simba bao la kusawazisha kwa mpira wa kona uliokwenda moja kwa moja wavuni na kuwaacha mabeki wa Yanga na kipa Ally Mustapha wasiamiani kilichotokea.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kubaki kileleni mwa ligi wakiwa na pointi 17, wakifutiwa na Stand United (12), Yanga ni tatu pointi 11, huku Azam ikiwa nafasi ya nne na pointi 10 kabla ya mechi zake za kesho.
Katika mchezo huo uliotawaliwa na ubabe, mwamuzi Martin Saanya alitoa kadi nyekundu kwa nahodha wa Simba, Jonas Mkude baada ya kiungo huyo kumkata mtama mwamuzi, pamoja na kucheza pungufu bado Simba ilifanikiwa kutuliza mashambulizi ya Yanga.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amesema mechi ni ngumu, timu yake ilicheza vizuri kipindi cha kwanza na kutumia vizuri nafasi waliyopata, lakini kipindi cha pili walipoteza mwelekeo.
Category: tanzania
0 comments