YANGA WA KIMATAIFA HAOOO KILELENI ... YAIPIGA TOTO MKONO MZIMA

Unknown | 7:06 PM | 0 comments

Tambwe amefunga bao la 17 leo Ligi Kuu
Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
SIMBA SC imeendelea kuwa dereva wa muda mfupi wa usukani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya leo kushushwa kileleni na watani zao, Yanga.
Yanga imerejea kileleni baada ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya ndugu zao, African Sports ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi wa leo, unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 50 baada ya kucheza mechi 21, huku Simba SC yenye pointi 48 za mechi 21 pia, ikiangukia nafasi ya pili na Azam FC inayobaki na pointi zake 47 za mechi 20, inabaki nafasi ya tatu.
Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na beki mzalendo, Kevin Yondan na washambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma, Mrundi Amissi Tambwe na Mzanzibar Matheo Anthony. 
Beki wa zamani wa Simba SC, Yondan maarufu kwa majina ya utani ‘Cotton Juice’ na ‘Vidic’ ndiye aliyefungua sherehe za mabao Jangwani, baada ya kufunga la kwanza dakika ya 32 kwa shuti kali akimalizia krosi ya kiungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima.
Donald Ngoma akafunga bao lake la 13 katika Ligi Kuu msimu huu dakika ya 37 kwa shuti pia, akimalizia krosi ya beki wa kulia aliye katika kiwango kizuri hivi sasa, Juma Abdul.
Kikosi cha Yanga kilichowafunga 5-0 African Sports leo

Amissi Tambwe naye akafunga bao lake la 16 msimu huu katika Ligi Kuu dakika ya 51 na kumfikia mpinzani wake katika mbio za ugungaji bora, Hamisi Kiiza wa Simba.
Mshambuliaji Matheo Anthony aliyetokea benchi kipindi cha pili akaifungia Yanga bao la nne dakika ya 58, akiunganisha krosi ya mchezaji mwenzake wa Zanzibar, beki Mwinyi Hajji Mngwali. 
Tambwe akajiweka kileleni mwa ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu baada ya kuifungia Yanga bao la tano dakika ya 72 kwa shuti kali, akifikisha mabao 17.
Baada ya mchezo huo, Yanga inatarajiwa kuondoka keshokutwa kwenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya wenyeji APR Jumamosi.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Vincent Bossou/paul nonga dk77, Pato Ngonyani, Deus Kaseke/Salum Telela dk61, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Matheo Anthony dk57, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima. 
African Sports: Kabali Faraji, Mwaita Ngereza, Hamza Kassim/Khalfan Twenye dk61, Juma Shemvuni, Rahim Juma, Ally Ally, Hussein Issa, Pera Mavuo, Rajab Isihaka, James Mendi na Omari Issa/Mohammed Mtindi dk73.

No comments:

POST A COMMENT

Note: Only a member of this blog may post a comment.
Pages 22123456 »

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments