YANGA YAPIGA MTU KAMA KAWA

Unknown | 11:22 AM | 0 comments

Tambwe & BusunguWachezaji wa Yanga wakishangilia goli.
Hans Mloli,Dar es Salaam
ULIDHANI Yanga imepotea? Usijidanganye, moto wa Yanga si wa kitoto, wakiamua kupiga wanapiga kweli, tena bila huruma. Jana maafande wa JKT Ruvu, waliuonja moto huo wa Jangwani baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Licha ya kumkosa mfungaji wao bora hadi sasa msimu huu, Amissi Tambwe, Yanga iliweza kupata ushindi huo mkubwa.Winga Simon Msuva aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 13 na kufikisha mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara. Mabao mengine yalifungwa na Mniger, Issofou Boubacar (dakika ya 44) ambaye lilikuwa bao lake la kwanza la ligi tangu ajiunge Jangwani, Donald Ngoma dakika ya 63 na Msuva akahitimisha kwa kufunga bao lake la sita kwenye ligi dakika ya 90.
Hata hivyo, JKT wangeweza kula hata bao tisa, kama Msuva angezitumia vizuri nafasi tano za wazi alizozipata ndani ya eneo la hatari. Lakini kipa wa JKT, Shaban Dihile, anastahili pongezi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga iendelee kujikita kileleni ikiwa na pointi 43, lakini Azam wana michezo mmoja mkononi huku wakiwa na pointi 42, sawa na Simba.
Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, alisema baada ya mchezo: “Nafurahi tumeshinda lakini tulikuwa na takriban wachezaji watano nje kutokana na mambo mbalimbali. Tulipoteza nafasi nyingi lakini mwisho tumeshinda. Bado tunahitaji ushindi zaidi kwenye mechi nyingine zilizobaki.”
Kwa upande wake, Kocha wa JKT, Abdallah Kibadeni, ambaye kikosi chake kipo katika hatari kubwa ya kushuka daraja baada ya kushinda mechi tatu tu kati ya 18 huku kikifungwa mechi 11, amesema: “Walituzidi sana Yanga, tulipungukiwa mbinu za kuwadhibiti. Karibu mabao yote tulifungwa kwa udhaifu. Tunahitaji kujipanga zaidi.”
Yanga iliwakilishwa na Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Salum Telela, Msuva, Haruna Niyonzima, Ngoma/Mwashiuya, Malimi Busungu/Paul Nonga na Boubacar/Deus Kaseke.
Baada ya mchezo wa jana, Yanga itakwenda kwenye michuano ya kimataifa halafu mechi inayofuata ya ligi itakuwa dhidi ya Simba Februari 20.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments