YANGA YAENDELEA KUTOA DOZI NENE

Unknown | 8:47 PM | 0 comments

Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM BIN ZUBERY
KAMA ilivyotarajiwa, Yanga imetinga Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, kufuatia ushindi wa 2-0 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya kushinda 1-0 katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita Mauritius, Yanga leo imemaliza kadhia kwa kuendeleza rekodi ya kushinda ‘mbili mbili’ kuanzia mechi na mahasimu wa jadi, Simba Jumamosi iliyopita na katikati ya wiki dhidi ya JKT Mlale katika mashindano ya nyumbani.  
Amissi Joselyn Tambwe, mshambuliaji wa zamani wa Simba SC na Vital’O ya kwao, Burundi aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya tatu kwa kichwa akimalizia krosi ya winga Simon Msuva.

Kikosi cha Yanga kilichoifunga cercle de Joachim 2-0 leo Uwanja wa Taifa

Malimi Busungu akapoteza nafasi tatu mfululizo, dakika ya tisa, alipounganishia nje pasi ndefu ya kiungo Deus Kaseke, dakika ya 39, alipounganishia nje tena kwa kichwa krosi ya Thabani Scara Kamusoko na dakika ya 44, alipopiga nje baada ya kugongeana vizuri na winga Simon Msuva hadi kwenye eneo la hatari la wapinzani.
Haikuwa ajabu kwa kupoteza nafasi zote hizo, Yanga wakienda kupumzika wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0 tu, lakini kipindi cha pili walifanikiwa ‘kuunenepesha’ ushindi wao kwa bao la ‘Rasta’ Kamusoko dakika ya 56 kwa shuti kali akiwa nje ya boksi, baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na beki Mwinyi Hajji Mngwali.
Paul Nonga naye aliyetokea benchi kipindi cha pili, aliunganishia nje krosi ya Kaseke dakika ya 52, kabla ya Tambwe naye dakika ya 54 kumbabatiza kipa Abrefa Godfrey Yaw shuti lake wakiwa wamebaki wawili wanatazamana. Tambwe tena dakika ya 71, akaunganishia juu ya lango krosi ya Mwinyi Hajji.
Kwa ujumla, Cercle walizidiwa na Yanga SC katika mchezo wa leo, ambao kama washambuliaji wake wangekuwa makini, wangeondoka na ushindi mkubwa zaidi.  Yanga sasa itakutana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland katika Raundi ya Pili.
Kikosi cha Yanga kilikuwa: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondani, Vincent Bossou, Mbuyu Twite/Pato Ngonyani dk46, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Malimi Busungu/Paul Nonga dk46 na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya dk76.
Cercle de Joachim: Abrefa Godfrey Yaw, Buckland Jimmy Hendrick/ Laretif Stan dk83, Balisson Paschal Damien, Natrey Isaac, Bazerque Desire, Permal Cedric, Langue Jean Anderson, Rasdarising Bhavish/Maguy Jacque Daniel dk78, Pithiaj Louis Fabien, Odame Abraham na Chiffone Louis Guiyano.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments