LEO NDIO LEO MTANANGE WA WATANI WA JADI SIMBA Vs YANGA
a Prince Akbar, DAR ES SALAAM
HATIMAYE ile siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu imewadia – ni leo Jumamosi ya Februari 27, 2016 ambayo inaikutanisha miamba ya soka nchini, Simba na Yanga.
Ni katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba wanashuka dimbani wakiwa kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zao 45 baada ya kucheza mechi 19, wakifuatiwa na Yanga SC wenye pointi 43 za mechi 18, wakati Azam FC inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake 42 za mechi 17.
Hiyo inamaanisha mchezo huo wa watani wa jadi ndiyo utaamua timu ya kutakaa kileleni baada ya mechi za mzunguko wa 20.
Washambuliaji vinara wa mabao, Hamisi Kiiza wa Simba kulia na Amissi Tambwe (kushoto) wanatarajiwa kuongoza safu za mbele za timu zao leo |
Simba SC imekuwa kambini Chuo cha Biblia eneo la Bigwa mkoani Morogoro tangu Jumapili ikitokea mkoani Shinyanga ambako ilishinda mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu, 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na 2-1 dhidi ya Stand United, wakati Yanga SC ilikuwa kisiwani Pemba, ambako iliwasili Jumapili ikitokea Mauritius ilikoshinda 1-0 katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim.
Simba SC walirejea Dar es Salaam usiku wa juzi, wakati Yanga SC waliwasili mchana na zote zimefikia katika hoteli za nyota tano katikati ya Jiji.
Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amekwepa kutanguliza majigambo kuelekea mchezo, wakati mpinzani wake, Mganda Jackson Mayanja hajasita kutamba atashinda hata 3-0. Mayanja anasema kwamba baada ya kuiona Yanga SC katika mechi kadhaa za hivi karibuni amegundua ni timu anayoweza kuifunga kwa urahisi.
Pluijm amewapa heshima yao Simba SC kwamba ni timu ambayo imeimarika kwa sasa na anaamini mchezo utakuwa mgumu hii leo na hasa akizingatia atawakosa mabeki wake wazoefu wa kati, Kelvin Yondani anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Ikumbukwe mara ya mwisho timu zilipokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Yanga SC ilishinda 2-0 Septemba 26, mwaka jana Uwanja wa Taifa, mabao ya Amissi Tambwe na Malimi Busungu.
Mayanja ameiongoza Simba SC kushinda mechi zote sita za Ligi Kuu tangu arithi mikoba ya Muingereza, Dylan Kerr Januari mwaka huu, wakati Pluijm ambaye yupo Yanga SC tangu mwaka 2014 amepoteza mchezo mmoja tu msimu huu akifungwa 2-0 na Coastal Union Januari 30, mwaka huu.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezeshwa na refa, Jonesia Rukyaa mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), atakayesaidiwa na Josephat Bulali wa Tanga, Samuel Mpenzu wa Arusha, Elly Sasii wa Dar es Salaam, atakayekuwa refa wa akiba, wakati Kamisaa atakuwa Khalid Bitebo Mwanza.
Vikosi vinatarajiwa kuwa; Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Mwinyi Mngwali, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke.
Simba SC; Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Juuko Murshid, Justice Majavbi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Ibrahim Hajib, Hamisi Kiiza na Awadh Juma.
Kwa ujumla Ligi Kuu inaendelea leo kwa michezo sita kuchezwa kwenye viwanja tofauti nchini, ukiwemo huo wa watani wa jadi.
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Mgambo JKT wataikaribisha Tanzania Prisons, Uwanja wa Kamabarage Shinyanga Stand United wataikaribisha JKT Ruvu, Uwanja wa Sokoine Mbeya – Mbeya City watakuwa wenyeji wa Azam FC, Uwanja wa Majimaji Songea, Majimaji wataikaribisha Mtibwa Sugar na Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Toto Africans watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar.
Kesho kutakuwa na michezo miwili ya kukamilisha mzunguko wa 20 wa ligi hiyo, kati ya Ndanda FC na African Sport Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Mwadui FC dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Ni Yanga tena, au Simba leo Uwanja wa Taifa? Dakika 90 zitatoa majibu. Na Bin inert blpg
Category: tanzania
0 comments