CHIPOLOPOLO WAIPIGA KAMOJA WARUNDI

Unknown | 9:30 PM | 0 comments

Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
ZAMBIA imevuna ushindi wa kwanza Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kuilaza Burundi 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Nyayo, Nairobi, jioni hii.
Bao pekee la mabingwa hao wa zamani wa Afrika, limefungwa na Festus Mbewe aliyeingia kuchukua nafasi ya Bornwell Mwape kipindi cha pili akimalizia pasi ya Felix Katongo dakika ya 64.
Kabaso Chongo wa Zambia kushoto akipambana na beki wa Burundi, Hakizimana Hassan katika mchezo wa leo wa Kundi B. Zambia ilishinda 1-0.

Ushindi huo, unaifanya Zambia iwe na pointi nne sawa na Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ambayo imeifunga Somalia 1-0 katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja huo huo leo.
Burundi inabaki na pointi zake tatu katika nafasi ya tatu, ambazo ilizivuna baada ya kuifunga Somalia 2-0 katika mchezo wa kwanza.  
Matokeo haya yanamaanisha mechi ya mwisho ya Stars na Burundi itakuwa kali kweli kweli, Bara ikihitaji japo sare na Burundi wakitaka lazima ushindi kufufua matumaini ya kusonga mbele.
Zambia itamaliza na Somalia ambayo mara nyingi huwa haikubali kupoteza mechi zote hadi sasa ikiwa imekwishafunga mechi zote mbili za awali na Burundi na Bara.
Kikosi cha Zambia kilikuwa; Nsabata Toaster, Bronson Chama, Justin Zulu, Chirstopher Munthali, Rodrick Kabwe, Bornwell Mwape/Festus Mbewe dk59, Sydney Kalume, Julius Situmbeko, Felix Katongo/Salulani Phiri dk90, Ronald Kampamba na Kabaso Chongo.
Burundi; Arakaza Arthur, Hakizimana Hassan, Hererimana Rashid, Hakizimana Issa, Nsabiyumva Frederic, Ndarusanze Claude, Ndikumana Yussuf, Duhayinavyi Gael/Nduwimana Jean dk73, Nduwarugira Christophe, Habonimana Celestin na Abdul Razak Fiston.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments