STARS YAIKOMALIA ZAMBIA

Unknown | 10:59 PM | 0 comments

Mrisho Ngassa akishangilia baada ya Said Morad  kuisawazishia Stars,

Na Mahmoud Zubeiry, Machakos
TANZANIA Bara, Kilimanjaro Stars imeanza taratibu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kutoa sare ya 1-1 na mabingwa wa zamani wa Afrika, Zambia au Chipolopolo kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos, Kenya.
Katika mchezo huo wa Kundi B, Zambia ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Ronald Kampamba dakika ya 41, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Felix Katongo.
Zambia walitawala zaidi mchezo huo kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi zaidi ya nne za kufunga, lakini sifa zimuendee kipa Ivon Philip Mapunda aliyeokoa michomo kadhaa ya hatari.
Kipindi cha pili, Stars ilibadilika mno kiuchezaji, japokuwa wachezaji waliomaliza kipindi cha kwanza ndiyo wote waliorejea kuanza ngwe hiyo ya lala salama.
Kutokana na mshambulizi mfululizo langoni mwa Zambia, Bara walipata kona dakika ya 48 ambayo ilikwenda kuchongwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kuunganishwa nyavuni na Said Morad kwa kichwa.
Baada ya bao hilo, Zambia walianza kuutafuta mpira kwa tochi na kama si umahiri wa kipa wao, Nsabata Toaster kuokoa hatari nyingi, Stars wangeweza kuondoka na ushindi. 
Kwa matokeo hayo, Burundi inaongoza kundi hilo baada ya kuifunga Somalia 2-0 katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo kwenye Uwanja huo.
Mabao ya Burundi yalifungwa na Abdoul Fiston dakika ya 40 na Nduwarugira Christopher dakika ya 55.
Mchezo wa pili wa Kundi B unatarajiwa kufanyika jioni hii kati ya Bara na Zambia kwenye Uwanja huo huo.


Kikosi cha Stars kilikuwa; Ivo Mapunda, Himid Mao, Erasto Nyoni, Said Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk89, Hassan Dilunga/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk85, Elias Maguri/Haroun Chanongo dk72, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments