MAJEMBE MATANO YANGA YAONGEZA MIKATABA, YONDANI AZIMA NDOTO ZA MSIMBAZI!!
Wachezaji
watano wa timu ya Young Africans wameongeza mikataba ya muda mrefu
ambapo sasa wataendelea kuitumikia klabu yenye maskani yake mitaa ya
Twiga/Jangwani mpaka mwaka 2016, hili limefanywa na uongozi kwa
mapendekezo ya benchi la ufundi.
Wachezaji
ambao mpaka sasa wameshaongeza mikataba ya kuitumikia klabu ya Young
Africans ni walinzi Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub “Cannavaro”
(2014-2016), kiungo Athuman Idd (2014-2016), mshambuliaji Saimon Msuva
(2014-2016) na Jerson Tegete (2014-2016).
Mwenyekiti
wa kamati ya usajili wa klabu ya Young Africans Abdallah Bin Kleb
amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza taratibu zote
na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka mwaka
2016.
“Tupo
katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine, mazungumzo
yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao tutakua
tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda
mrefu “alisema Bin Kleb.
Wakati
huo huo kikosi cha Young Africans leo kimeanza mazoezi asubuhi katika
uwanja wa Bora – Mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa hisani
dhidi ya Simba SC Disemba 14, 2013, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya
Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Klabu Bingwa
Afrika.
Aidha
Uongozi wa klabu ya Young Africans unampa pongezi beki wake wa kati
Kelvin Patrick Yondani mchezaji bora wa mwaka 2012/2013 kwa kuteuliwa
kuwa nahodha mpya wa timu ya Taifa Tanzania bara (Kilimanjaro stars)
inayokwenda kushiriki mashindano ya Chalenji jijini Nairobi.
Kelvin
Yondani ametambulishwa rasmi leo na kocha mkuu wa timu ya Taifa Kim
Poulsen kwa waandishi wa habari katika hafla ya kuwaaga wachezaji wa
timu ya Taifa wanaokwenda nchini Kenya katika hoteli ya Accomondia eneo
la gerezani jijini Dar es salaam.
Tunapenda
kumpa pongezi kijana wetu, mchezaji wetu Yondani kwa kupewa nafasi hiyo
kubwa katika timu ya Taifa, tunamtakia kila la kheri na awe kiongozi
bora kwa wachezaji wenzake na kuiwakilisha vizuri nchi yetu na timu yake
ya Young Africans.
CHANZO: YOUNG AFRICANS SC OFFICIAL WEBSITE
Category: tanzania
0 comments