KILIMANJARO STARS YATUA SALAMA NAIROBI TAYARI KUWANIA CHALLENGE CUP
Timu
ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya
tayari kwa mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27
mwaka huu) katika Uwanja wa Nyayo.
Kilimanjaro
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku
kwa ndege ya RwandAir, na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko
katikati ya Jiji la Nairobi.
Kwa
mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, Kilimanjaro Stars leo
(Novemba 26 mwaka huu) ni mapumziko ambapo kesho itafanya mazoezi
kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia itakayochezwa Novemba
28 mwaka huu Uwanja wa Machakos.
MECHI YA TANZANITE SASA KUCHEZWA DAR
Mechi
ya kwanza ya raundi ya michuano ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa
wanawake chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini
iliyokuwa ichezwe Mwanza sasa itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Baada
ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), imebainika uwanja huo unatakiwa ufanyiwe marekebisho
ambayo hayawezi kuwahi Desemba 7 mwaka huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo
inatakiwa kuchezwa.
Vyumba vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa.
WANNE WASHINDA UCHAGUZI CECAFA
Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata
wajumbe wapya wa wanne wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya
leo (Novemba 26 mwaka huu) hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi
huo ulifuatiwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake
Leodegar Tenga na kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.
Rais
wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA),
Lawrence Mulindwa ndiye aliyeongoza katika uchaguzi huo ambapo
wasimamizi walikuwa Bwalya na Maradas.
Mulindwa
alipata kura zote 12 na kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10),
Abdigaani Saeb Arab wa Somalia (9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8).
Atta, Arab na Gisanura walikuwa wakitetea nafasi zao.
Walioshindwa
ni Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor
aliyepata kura tano na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya
(FKF), Sam Nyamweya aliyepata kura nne.
MICHUANO YA UHAI YAHAMIA CHAMAZI
Michuano
ya Kombe la Uhai imeingia hatua ya robo fainali ambapo sasa mechi
zinachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya
Jiji la Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa wameathirika kutokana na uamuzi huo.
Category: tanzania
0 comments