WANASOKA WENYE KASI ZAIDI DUNIANI HAWA HAPA

Unknown | 8:56 AM | 0 comments

 


VALENCIA


 Na Saleh Ally
Mnyama mwenye kasi zaidi kuliko mwingine yoyote duniani ni chui aina ya Cheetah ambaye anakimbia kasi ya maili 64 au kilomita 104 kwa saa ambayo ni mara mbili na ushee zaidi ya binadamu mwenye kasi zaidi.

Binadamu mwenye kasi zaidi ni mwanariadha wa Jamaica, Usain Bolt, ambaye ameweka rekodi ya kukimbia kilomita 37.58 kwa saa. Aliweka rekodi hiyo katika mashindano ya ubingwa wa dunia hivi karibuni nchini Urusi.
Katika soka pia kuna watu wenye kasi kubwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limetoa rekodi zake kuonyesha wachezaji gani wana kasi zaidi ya wengine.
Winga au kiungo wa Manchester United, Antonio Valencia,  ndiye aliyeshika nafasi hiyo kutokana na data za wataalamu wanaofanya tathmini za shirikisho hilo kubwa zaidi la soka duniani.
Valencia ambaye hana sifa kubwa kwa mashabiki lakini amekuwa chachu kubwa ya ushindi wa Manchester United inapocheza mechi zake, ana kasi ya kilomita 35.1 kwa saa. Ingawa hajamfikia Bolt, lakini hakuna mwanasoka mwingine anayemfikia.
Gareth Bale ambaye ametua Real Madrid akitokea Tottenham anashika nafasi ya pili akiwa na kasi ya kilomita 34.7 kwa saa na ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi katika La Liga.
Baada ya hapo ni winga mwenye kasi wa Tottenham, Aaron Lenon, ambaye ana kasi ya kilomita 33.8 kwa saa akiwa amemzidi Cristiano Ronaldo kwa pointi mbili tu.
Ronaldo aliyekuwa mchezaji mwenye kasi zaidi La Liga kabla ya kutua Bale, anashika namba nne katika data hizo za Fifa akiwa na uwezo wa kukimbia kilomita 33.6 kwa saa na Theo Walcott wa Arsenal anafunga tano bora kwa mwendo wa kilomita 32.7 kwa saa.
Tayari imezua mjadala mkubwa wengi wakiwa hawaamini kama kweli Valencia ndiye mwenye kasi zaidi, lakini Fifa imeshikilia hilo huku ikitaka watu wahakikishe kwa utaalamu na si maneno.
Premiership imekuwa ligi yenye wachezaji wengi zaidi wenye kasi duniani kwa kuwa katika tano bora ina wachezaji watatu na kumi bora inao wanne wakati La Liga inashika nafasi ya pili kwa kuwa na wawili tano bora na wanne kumi bora.
Lakini Premiership inaonekana iko juu zaidi kwa kuwa hata wachezaji wenye kasi zaidi wa La Liga ambao ni Bale na Ronaldo, wote wametokea England.
Bundesliga inashika nafasi ya tatu, haina mchezaji katika tano bora lakini imeingiza Arjen Robben na Frank Ribery wanaoshika nafasi ya nane na tisa. Ligi nyingine kubwa za Ufaransa na Italia, hazijaingiza mchezaji katika hatua ya 10 bora.
Kingine ambacho kinavutia zaidi ni kwamba, 10 bora ya wenyewe inaonyesha hivi, wote ni washambuliaji au viungo wa pembeni na hakuna beki.
Kama ni hivyo, vipi mabeki, na wanaweza vipi kuwadhibiti wasilete madhara? Jibu lake ni hili, katika soka, kasi haiwezi kuwa kila kitu na kuna mbinu na mambo mengi yanayotakiwa zaidi ya kasi pekee.
Kumi bora ya wenye mwendo kasi duniani:
1. Antonio Valencia          (Manchester United) 35.1 km / h
2. Gareth Bale                    (Real Madrid) 34.7 km / h
3. Aaron Lennon                 (Tottenham Hotspur) 33.8 km / h
4. Cristiano Ronaldo         (Real Madrid) 33.6 km / h
5. Theo Walcott                 (Arsenal FC) 32.7 km / h
6. Lionel Messi                   (FC Barcelona) 32.5 km / h
7. Wayne Rooney              (Manchester United) 31.2 km / h
8. Franck Ribery                 (Bayern Munich) 30.7 km / h
9. Arjen Robben                 (Bayern Munich) 30.4 km / h
10. Alexis Sánchez             (FC Barcelona) 30.1 km / h

Share story hii kupitia>>>>>> :
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Category:

0 comments